WAHITIMU KUTOKA CHUO KIKUU CHA DODOMA |
WASOMI watakaohitimu
vyuo vya elimu ya juu nchini kuanzia mwaka huu watakopeshwa mabilioni ya fedha
ili waanzishe miradi itakayowawezesha kujiajiri. Hatua hiyo ni matokeo ya Programu
ya Wizara ya Kazi na Ajira inayolenga kukuza ajira kwa vijana wahitimu wa vyuo
hivyo, kwa kushirikiana na vya elimu ya juu, taasisi za fedha na wabia wa
maendeleo.
Akizungumza Dar es
Salaam jana, Msemaji wa Wizara hiyo, Ridhiwani Wema alisema, Sh bilioni 54
zitahitajika kufanikisha miradi 1,000 itakayotekelezwa kwa awamu tatu kwa miaka
mitatu ya utekelezaji. Kwa mujibu wa Wema, kati ya fedha hizo, Sh bilioni 4.4
ni za mafunzo na kuandaa vijana ili wakopesheke na Sh bilioni 50 zitakuwa
dhamana.
“Lengo la kuanzisha
programu hii ni kuongeza fursa za ajira 30,000 za moja kwa moja kwa wasomi hao
kwa kipindi hicho. Tunaamini miradi watakayoanzisha itafanya wajiajiri na
kuajiri wengine.
"Katika
kuhakikisha programu hii inafanikiwa, Serikali imekubaliana na Benki ya CRDB
kutoa mikopo kwa vijana, mara utekelezaji utakapoanza rasmi. Utaanza kwa
kuendeleza programu ya mfano iliyoanzishwa na Idara ya Kilimo, Uchumi na
Biashara katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)," Wema alisema.
BAADHI YA WAHITIMU WA CHUO KIKUU CHA WAISLAM MOROGORO |
Alisema, baada ya hapo,
wahitimu wa vyuo vingine vya elimu ya juu nao watafikiwa na kuandaliwa vizuri
kwa mafunzo ili wawe wajasiriamali kupitia miradi watakayoianzisha kwa kutumia
mikopo watakayopewa. Wema alifafanua kuwa wahusika watalazimika kuandika
mapendekezo ya miradi yao ambayo yataangaliwa na kupangiwa kiasi cha fedha, ili
waweze kukopeshwa tayari kwa kuanza kuitekeleza.
"Miradi
itakayoanzishwa itatoa mnyororo mzima wa thamani, kwa mfano mradi wa alizeti na
ukamuaji mafuta. Tumejiridhisha kuwa miradi hiyo itapunguza wimbi la vijana
kukimbilia mijini, kwa sababu itakuwa ikitekelezwa katika maeneo watakakokuwa
wahitimu hao ambayo si ya mjini pekee," alisema.
Wema alifafanua kuwa
katika awamu ya kwanza vijana 600 kutoka SUA watahusika kumiliki miradi 200 ya
kujiajiri na kuajiri wahitimu wengine 5,400, wakati katika awamu ya pili,
vijana 900 kutoka vyuo vingine wataanzisha miradi 300. Kwa maelezo yake, awamu
ya tatu itahusisha wahitimu 1,500 wa vyuo vingine ikiwamo VETA itakayokuwa na
miradi 500 itakayozalisha ajira 13,500.
"Hivyo ndivyo
tutakavyotumia programu hii kupunguza tatizo la ajira na kuhakikisha
wanaoandika mapendekezo yenye ushawishi na yanayoelezea miradi inayotekelezeka
watakopeshwa," alisema na kuongeza kuwa muda utakapofika, wahitimu
wataandikishwa na kutambuliwa kupitia mikoa na wilaya wanamoishi.
Kuhusiana na Utapeli wa
AJIRA, wakati mikakati ya ajira ikiwekwa ili kukomboa vijana wasomi nchini,
Jeshi la Polisi Dodoma linamshikilia Mariam Tawakali (28) akidaiwa kutapeli
wahitimu wa vyuo vikuu kwa ahadi ya kuwapa kazi ya kuandikisha wananchi
wanaotarajiwa kupewa vitambulisho vya uraia chini ya Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa (NIDA).
Hayo yalithibitishwa
jana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime akisema Mariam
alikamatwa juzi katika Barabara ya Sita, Dodoma, baada ya Polisi kupata taarifa
kutoka kwa raia wema.
Alisema mtuhumiwa
alikutwa na vitambulisho vitano vyenye majina tofauti ya Mariam Tawakali na
Monica Emmanuel Ngaso (28), mkazi wa Nkuhungu, Dodoma.
Miongoni mwa
vitambulisho hivyo ni cha Mkutano Mkuu wa CCM, wa Novemba 11-13, mwaka jana
ambapo kazi yake ilionesha kuwa ni mhudumu.
Kingine ni cha kampuni
ya Thaker Singh Coast Action chenye jina la Monica Emmanuel Ngaso, kazi Katibu
Muhtasi, nacho kitambulisho cha New Dodoma Hotel chenye jina la Mariam Tawakal
kazi yake Katibu Muhtasi na cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima chenye jina la
Mariam Tawakali, kikionesha ni mwalimu wa taasisi hiyo kijijini Chamwino.
Kamanda Misime alisema
Mariam alitangazia wananchi, kwamba kazi ya kuandikisha vitambulisho vya uraia
kwa Dodoma itaanza mwezi ujao.
Pia waliwaeleza kuwa
atakayehitaji kazi hiyo awasilishe maombi kwake akiambatanisha vyeti vya elimu
ya sekondari au chuo, picha za vitambulisho na fedha taslimu Sh 110,000 za
kiingilio. Aidha, aliwaambia atakayepata nafasi atalipwa mshahara wa Sh 400,000
kwa mwezi kwa miezi mitatu ambapo kazi hiyo itakuwa imekamilika.
Alisema mtuhumiwa huyo
alifanikiwa kukusanya vyeti, picha na fedha kwa wananchi 29 wengi wao wakiwa
wahitimu wa vyuo vikuu mwaka huu.
Kamanda Misime alisema
Polisi inatoa hadhari kwa wananchi kuwa makini na wanaofanya vitendo hivyo na
kuwataka kutoa taarifa mapema wanapotilia shaka watu wa aina hiyo ili hatua za
kuwadhibiti zichukuliwe mapema.
Alitaka wananchi
kuelewa kuwapo matapeli wanaobuni miradi ya kujipatia fedha kwa udanganyifu na
kuwataka kuchukua hadhari mapema kwa kukataa kurubuniwa ajira na kutoa fedha
bila kuthibitisha.
Alisema Polisi
inafuatilia kuona uhalali wa vyeti vya wanafunzi hao wa vyuo vikuu na kuona ni
kosa gani Mariam atashitakiwa nalo. Pia alitaka waliotapeliwa kufika Polisi
kutoa ushahidi kabla ya kesi haijafikishwa mahakamani.
PICHA YA PAMOJA NA WAHITIMU WA CHUO CHA MUM |
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako