Thursday 12 February 2015

FAIDA YA TUNDA NANASI



Moja kati ya matunda ambayo yanapendwa zaidi ni tunda la nanasi, linapendwa zaidi kutokana na ladha nzuri na utamu ambao unatokana na sukari iliyoko ndani ya tunda hili ambapo inafanya tunda hili kuwa moja kati ya matunda ambayo yanatumika sana kwa kutengeneza juice.

Hata hivyo baada ya kusoma taarifa hii ya utafiti utapata sababu zaidi za kupenda kula mananasi, zipo faida nyingi sana kwenye mwili wa mwanadamu faida ambazo ni za kiafya zaidi.

Mananasi yana virutubisho hivi muhimu kwa mwili wa mwanadamu.
Mananasi ni chanzo muhimu sana cha vitamin pamoja na madini ambayo yanasaidia kuimarisha afya ya mwanadamu ambazo ni kama vile Thiamin, Riboflavin, Vitamini B-6 , Folate , Acid ya Pantothetic pamoja na madini ya Magnesium, manganese na potasia.
Katika hesabu za kitabibu, kipande kimoja cha nanasi kinatosha kuongeza 131% yavitamin c ambayo mwili wako unaihitaji kwa siku moja.

Mananasi husaidia kutibu vidonda na uvimbe.
Moja kati ya vurutubisho vilivyoko ndani ya nanasi kinaitwa Bromelain, husaidia sana kuondoa maumivu kwenye viungo, kupunguza hali ya uvimbe kwenye tezi  na hata kupunguza uvimbe wa kawaida ambao umetokea ndani ya mwili na pia humsaidia sana mtu akiwa amefanyiwa upasuaji.

Mananasi husaidia Mfumo wa usagaji (Mmeng’enyo) wa chakula.
Manansi yana virutubisho vya kambakamba (fibre) ambavyo husaidia sana kwenye kusagwa kwa chakula mwilini, kirutubisho cha Bromelain pia husaidia kwneye kusaga chakula tumboni kwa kusaidia kuvunja vile vipande vya protini.
Manufaa ya nanasi kwenye ngozi
Vitamini C ipatikanayo kwenye mananasi husaidia sana kuipa ngozi mng’ao ambao unahitajika, mishipa midogo ya damu pia hufaidika sana kutokana na mananasi pamoja na viungo vingine vya mwili na mifupa pia.

Manufaa ya nanasi kwenye mifupa
Mananasi yana madini aina ya Manganese ambayo husaidia kuzalisha nishati mwilini huku ikisaidia kutoa ulinzi kwa seli za mwili wa mwanadamu.
Madini haya yanasaidia sana ufanyaji kazi wa madini mengine na virutbisho kamaThiamine na Biotin ambayo kazi yake kubwa ni kusaidia kufanya mifupa kuwa migumu na yenye afya zaidi na pia husaidia kuyayusha vyakula vyenye mafuta.

Mananasi husaidia Macho .
Tunda aina ya nanasi lina vitamin A pamoja jna kirutubisho aina ya Beta-Caroteneambavyo kwa pamoja husaidia mfumo wa kinga ya mwili na afya ya macho.
 Mananasi hutoa nguvu na nishati na kushusha shinikizo la damu.
Mananasi ya kiwango kikubwa cha Vitamini B1 na B6 ambavyo ni vyanzo muhimu sana vya nishati pamoja na kuvunjavunja sukari kwenye mfumo wa usagaji wa chakula.
Madini ya shaba pia yanapatikana kwenye mananasi yanasaidia sana kutoa afya kwa seli nyekundu zinazosaidia kutengeneza damu na madini ya potasia ambayo yanasaidia kuweka mapigo ya moyo sawa na kushusha shinikizo la damu.

Monday 9 February 2015

HONGERA IVORY COAST KWAKUWA MABINGWA WAPYA WA AFCON


Timu ya taifa ya soka ya Ivory Coast imefanikiwa kuunyakua ubingwa wa mataifa ya Afrika kwa mara ya pili, baada ya kuibwaga Ghana 'Black Stars' katika mechi ya fainali iliyochezwa nchini Equatorial Guinea. Kwenye pambano hilo kali na la kusisimua  lilimalizika katika dakika 90 za mchezo, huku timu zote mbili zikitoka sare ya bila ya kufungana.
 Muda wa dakika 30 za nyongeza nao haukuweza kumtoa mshindi wa pambano hilo. Baada ya kumalizika dakika 120 za mchezo, ulichukuliwa uamuzi wa kupigiana penalti  tano – tano, na hapo ikajirudia historia ya fainali ya mwaka 1992.
 Ivory Coast ilianza kupoteza penalti zake mbili, huku Ghana wakiwa na matumaini ya kuibuka na ushindi, lakini Ivory Coast ilianza kujirekebisha katika upigaji wa penalti, na Ghana nao wakaharibu mikwaju yao miwili, lakini baada ya kuendelea michomo ya funga nikufunge, hatimaye kipa wa Ivory Coast alizuia mkwaju wa kipa wa Ghana, na kutandika mkwaju wa tisa na kuibeba Ivory Coast kwa ushindi wa mabao 9-8.
Mchuano huo ulirejesha historia ya fainali ya mwaka 1992, ambapo Ivory Coast iliutwaa ubingwa huo kwa kuifunga Ghana kwa mikwaju ya penalti 12 kwa 11. Ghana imeshalinyakua kombe la mataifa ya Afrika mara tano. Siku ya Jumamosi, ilichezwa mechi ya kumtafuta mshindi wa tatu wa michuano hiyo kati ya wenyeji Equatorial Guinea ilipokamuana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo Kongo ilishinda kwa penalti 4-2.

Friday 6 February 2015

UWANJA WA MALABO WAGEUKA VITA BAADA YA WENYEJI GUINEA KUPIGWA 3 BILA NA BLACK STARS



NDOTO za wenyeji Equatorial Guinea kunyakua Kombe la Mataifa ya Afrika zimeyeyuka usiku wa jana baada ya kufungwa mabao 3-0 na Ghana Uwanja wa Malabo.

Black Stars inayofundishwa na kocha wa zamani wa Chelsea, Avram Grant ilipata mabao yake kupitia kwa Jordan Ayew kwa penalti dakika ya 42, Mubarak Wakaso dakika ya 45+1 na Andre Ayew dakika ya 75.

Baada ya bao la tatu, huku Ghana wakiendelea kuwashambulia wenyeji, zikiwa zimesalia dakika nane mchezo kumalizika, mashabiki wa Guinea walianza kurusha chupa uwanjani na pia kuwapiga nazo mashabiki wa Ghana, ambao walilazimika kuvamia uwanjani kunusuru maisha yao.

Polisi walilazimika kutumia hadi helikopta kuwaondoa uwanjani mashabiki wa Guinea na baada ya nusu saa hali ilipotulia Uwanja ulikuwa kama mtupu na refa Eric Castane akamalizia mchezo.  

Ghana sasa itamenyana na Ivory Coast katika fainali ya AFCON 2015 Jumapili, wakati hatma ya wenyeji na mchezo wa mshindi wa tatu dhidi ya DRC haijajulikana, kwani kuna uwezekano wakapewa adhabu kali na CAF. 

Thursday 5 February 2015

GERRARD ACHEZA MECHI YA MIA 7 WAKATI LIVERPOOL WAKIIUA BOLTON 2 - 1



LIVERPOOL imetinga Raundi ya Tano ya Kombe la FA baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Bolton Wanderers  hapo jana.

Eidur Gudjohsen aliifungia Bolton bao la kuongoza kwa  mkwaju wa penalti dakika ya 59, baada ya kinda wa miaka 19, Zach Clough kuchezewa vibaya na beki wa Liverpool, Martin Skrtel ndani ya 18

Raheem Sterling akaisawazishia Liverpool dakika ya 85, kabla ya Philippe Coutinho kufunga goli la ushindi dakika ya 90. 

KIUNGO Steven Gerrard amekuwa mchezaji wa tatu wa Liverpool kutimiza mechi 700 kihistoria baada ya kuichezea timu hiyo jana ikishinda 2-1 dhidi ya Bolton katika mechi ya marudio Raundi ya Nne ya Kombe la FA.
Gerrard, ambaye maisha yae yote amecheza Liverpool pekee, alifurahia mafanikio yake hayo kwa kuvaa kiatu maalum kilichoandikwa 700 nyuma pamoja na majina ya mabinti zake, Lilly na Lexie.

Bolton ililazimika kucheza pungufu kwa dakika 20 za mwisho baada ya mchezaji wake, Neil Danns kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na Liverpool sasa itamenyana na Crystal Palace katika Raundi ya Tano.

YANGA YABANIWA NA TFF



SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limekataa ombi la Yanga SC kutaka mchezo wao na Mtibwa Sugar uahirishwe ili wapate fursa nzuri ya maandalizi ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya BDF XI ya Botswana.

Na kwa sababu, hiyo Yanga SC wanaondoka asubuhi ya leo kurejea kambini kwao, Bagamoyo kuendelea na maandalizi ya mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Yanga SC watacheza mechi ya tatu ndani ya wiki moja Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya mabingwa wenzao wa zamani wa Ligi Kuu, baada ya Jumapili iliyopita kulazimishwa sare ya 0-0 na Ndanda FC na jana kushinda 1-0 dhidi ya Coastal Union.

Yanga SC ilipanda kileleni mwa Ligi Kuu jana kufuatia ushindi huo wa ugenini, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa kutimiza pointi 22 baada ya kucheza mechi 12, moja zaidi ya mabingwa watetezi, Azam FC wanaoshika nafasi ya pili kwa point 21.

Shujaa wa pointi tatu za Yanga SC jana alikuwa ni Nahodha Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’, aliyefunga bao hilo pekee mapema tu kipindi cha kwanza, baada ya kupanda kwenda kusaidia mashambulizi.

Ilikuwa ni dakika ya 12 ya mchezo, wakati Cannavaro alipomalizia kwa kichwa mpira wa kurushwa wa beki Mbuyu Twite na kuipandisha kileleni Yanga SC.

Baada ya mchezo na Mtibwa Sugar Jumapili, Yanga SC itakwenda kuweka kambi visiwani Zanzibar kujiandaa na mchezo wa kwanza, Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho Afrika.
@@@@@@@@@@@@@@@