Wednesday 30 October 2013

YAYA TOURE AZURU KENYA


 
Mchezaji maarufu wa timu ya Manchester City Yaya Toure, amewasili mjini Nairobi Kenya kwa uzinduzi wa muungano mpya wa kukabiliana na uwindaji haramu kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mazingira (UNEP).

Muungano huo umeanzishwa ili kukabiliana na uwindaji haramu wa wanyama pori haswa Ndovu ambao wanakabiliwa na tisho la kudidimia kutokana na uwindaji haramu barani Afrika.

Toure, mshindi wa tuzo la mchezaji soka bora zaidi Mwafrika kwa miaka miwili mfululizo, 2011 na 2012 ataeleza kwanini amekubali kushirikiana na muungano huo kupambana dhidi ya uwindaji haramu na nini hasa jukumu lake.

Anatarajiwa kuongea na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa mataifa katika mtaa w akifahari wa Gigiri, Nairobi.
Wengine watakaozungumza ni Achim Steiner mkurugenzi mkuu wa shirika la UNEP pampja na mkurugenzi wa shirikisho la kandanda la kenya Sam Nyamwea.

TUTAJITOA EAST AFRIKA - TANZANIA


 
Serikali ya Tanzania imesema inatafakari ushiriki wake ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na inaweza kujitoa ndani ya Jumuiya hiyo iwapo itaendelea kutengwa katika baadhi ya vikao.
Aidha imesema Tanzania haitambui vikao vinavyofanywa na nchi tatu zilizopo ndani ya Jumuiya hiyo ambazo zimekuwa zikizitenga Tanzania na Burundi.
Waziri anayehusika na masuala ya Afrika Mashariki wa Tanzania Samwel Sitta ameliambia Bunge la Tanzania kuwa makubaliano ya vikao hivyo vinavyofanywa na nchi za Kenya, Rwanda na Uganda yatatekelezwa na nchi hizo zinazofanya vikao hivyo kwa sababu vinafanyika nje ya utaratibu wa mkataba wa jumuiya hiyo.
Katika mikutano iliyofanyika hivi karibuni Tanzania na Burundi hazikualikwa kwenye vikao hivyo.
Kwa mujibu wa Waziri Sitta mikutano ya wakuu wa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ambayo ilianza kwa kuitenga Tanzania ilifanyika Entebbe nchini Uganda mwezi Juni mwaka huu na kufuatiwa na mkutano wa pili uliofanyika Agosti mwaka huu huko Mombasa nchini Kenya ambapo nchi hizo tatu bila kuishirikisha Tanzania walizungumzia uanzishaji wa himaya moja ya forodha.
Mambo mengine waliyozungumza wakuu hao ilikuwa uanzishaji wa visa moja ya utalii kwa nchi zao na matumizi ya vitambulisho vya uraia ambavyo vitatumika kama hati za kusafiria miongoni mwa nchi hizo.

Aidha Waziri Sitta amesema ndani ya mikutano hiyo pia walizungumzia kuanzisha mchakato wa kuanzisha shirikisho la nchi hizo.
Tayari Tanzania imeanza mazungumzo na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuangalia ni kwa namna gani zitaanzisha ushirikiano nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kama zinavyofanya nchi za Rwanda, Uganda na Kenya.

WATU 11 WAFARIKI KATIKA AJALI ILIYOHUSISHA TRENI NA BASI KENYA


  
Watu 11 wamethibitishwa kufariki katika ajali iliyohusisha treni na basi iliyokuwa imewabeba watu wakielekea kazini katika mtaa wa Umoja viungani mwa mji wa Nairobi.
Basi hilo linayoaminika kuwa na watu 34 liligongwa na treni kwenye njia ya reli kuelekea mjini. Kwa mujibu wa shirika la Red Cross, idadi ya majeruhi imefika 34 na wamepelekwa katika hospitali kuu ya Kenyatta.
Baadhi ya waliojeruhiwa wanasemekana kuwa katika hali mbaya.
Walioshuhudia ajali hiyo wanasema kuwa basi hilo lilisukumwa umbali wa mita hamsini baada ya kugongwa kwa upande.

Inaarifiwa watu sita walifariki papo hapo na wengine wawili kufariki baadaye kutokana na majeraha waliyoyapata.
Wengine wengi wamejeruhiwa kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu.
Mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP aliyeshuhudia ajali hiyo alisema kuwa basi iliharibiwa vibaya baada ya kugongwa kwa upande na treni ihiyo ilikuwa inasafiri kwa kasi kubwa.
Ajali hiyo imetokea asubuhi wakati wa msongamano wa watu na magari huku watu wengi wakiwa katika haraka kuelekea kazini.

DIAMOND AZUA TAFRANI KWA KUTAKA KUINGIA NA JENEZA KWENYE ONESHO LA FIESTA


STAA wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ ambaye hakaukiwi na stori, safari hii amekuja na mpya baada ya kuibuka na jeneza lenye msalaba ambalo limeibua maswali mazito, Risasi Mchanganyiko linakupasha.
Diamond ambaye wimbo wake mpya wa ‘Number One’ upo katika chati ya juu katika muziki huo, usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita aliingia na jeneza hilo katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar na kusababisha maswali mengi tata kutoka kwa mashabiki waliojazana kwenye onesho la Serengeti Fiesta 2013.
ILIKUWA SAPRAIZI
Mapaparazi wa Risasi Mchanganyiko waliokuwa wamejaa katika viwanja hivyo wakihakikisha wananasa matukio muhimu hasa yale ‘exclusive’, walipenyezewa mapema kuhusu Diamond kuingia na jeneza.
Mtoa habari alisema Diamond aliingiza jeneza viwanjani humo kwa lengo la kupanda nalo jukwaani wakati akiimba wimbo wake uitwao Nikifa Kesho ambao mashabiki wake wengi wanasema amejichulia kifo.
Kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini, mtoa habari huyo ambaye ni mtu wa karibu na Diamond alisema:
“Diamond amekuja na jeneza, limefichwa kule nyuma wanakobadilishia nguo wasanii, atapanda nalo jukwaani. Anataka kuwafanyia sapraizi mashabiki wake.”

SAPRAIZI YAKWAMA
Hata hivyo, baada ya matatizo ya kiufundi yaliyojitokeza, Diamond hakuweza kupanda jukwaani Jumamosi usiku huo na badala yake akatakiwa kupanda kesho yake Jumapili ambapo pia hakulitumia jeneza hilo kama mawazo yake ya awali yalivyokuwa.
Mapaparazi wetu walisaka sehemu lilipohifadhiwa jeneza hilo na kufanikiwa ambapo pia walikuta baadhi ya watu wakilishangaa na kuulizana maswali.

MASWALI TATA
Nurdin Ali, mkazi wa Mbagala, Dar aliyeliona jeneza la Diamond alisema:
“Mimi namkubali sana huyu bwana mdogo lakini sasa mambo ya majeneza jukwaani ya nini tena?

“Sikubaliani na hili suala. Hata wimbo wake wa Nikifa Kesho sioni kama una mantiki. Ni kama tu anajitabiria kifo. Anapita mlemle alimopita marehemu Kanumba, maana naye aliimba wimbo akielezea itakavyokuwa siku akifa, ikawa kweli.

“Lakini Diamond amekwenda mbele zaidi kwa kuamua kuja na jeneza kabisa stejini. Sijui amenunua au amekodisha, ila sikubaliani naye hata kidogo.”

MATUMIZI YA JENEZA
Mwingine aliyekataa kuandikwa jina lake gazetini alisema:
“Halafu kama lengo lake lilikuwa kuonesha uhalisia wa kifo katika wimbo wake, kwa nini asingekuja na jeneza la imani yake? Angalia, jeneza lina msalaba ambao unakubalika katika imani ya Kikristo, kwa nini asije na jeneza la Kiislamu au sanduku ambalo halina msalaba?”

Akaongeza: Au inawezekana huyu jamaa anataka kubadili dini ili aoane na Penny (Penniel Mungilwa) ambaye ni Mkristo kwa sababu huku ni kukana imani yake kimyakimya.”

ALIWAHI KUTANGAZA KUJENGA MSIKITI
Shabiki mwingine alikwenda mbali zaidi na kusema kama Diamond ni muumini mzuri wa Kiislamu tena mwenye lengo la kujenga msikiti kama alivyowahi kutangaza siku za nyuma, anatakiwa kutofungamana kabisa na ishara zinazoonesha anaunga mkono imani nyingine.
“Anapaswa kuwa makini na mambo yake na awe na washauri wazuri, vinginevyo atakuwa anafanya mambo yanayoibua maswali mengi kwa jamii inayomwamini,” alisema shabiki huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Jennifer.
HUYU YUPO TOFAUTI
Shabiki aliyejitambulisha kwa jina la Hamadi Hajj (34) mkazi wa Kijitonyama, Dar alisema:
“Hakuna uhusiano wowote kati ya hili jeneza na mambo ya kubadilisha dini au kuiunga mkono. Kikubwa ni lengo alilotaka litimie.
“Ukiachana na hilo, mambo mengine yako wazi jamani. Upatikanaji wa majeneza ya Kikristo ni rahisi zaidi tofauti na ya Kiislamu. Wabongo wanapenda sana kukuza mambo,”  alisema Hajj.

HUKU RISASI, KULE DIAMOND
Siku hiyohiyo, usiku huohuo, mapaparazi wetu walimbana Diamond kuhusu kutinga Leaders na jeneza ambapo alijitetea hivi:
“Ni swaga tu zile.”
Alipobanwa zaidi na kuulizwa ni swaga gani zinazochanganywa na vitu vinavyoashiria huzuni na imani ambayo si yake, alisema:
“Nilitaka kuwafurahisha mashabiki wangu na kuwapa uhalisia wa ule wimbo wangu wa Nikifa Kesho, sikuwa na nia ya kukashifu imani ya mtu.”

FIESTA PART II
Baada ya shoo yake kushindikana na kuhamishiwa siku iliyofuata (Jumapili), timu yetu ilitinga viwanjani hapo ili kujua kama Diamond angepanda na jeneza hilo kama alivyotarajia lakini jeneza halikuwepo eneo lilipohifadhiwa awali.
Diamond alipofuatwa na kuulizwa kama mpango wake bado uko palepale, alijibu:

“Lile jeneza nilipanga kupanda nalo jukwaani wakati nikiwa naimba wimbo wangu wa Nikifa Kesho lakini kwa bahati mbaya sikuweza kupanda kuimba kutokana na matatizo ya kiufundi, leo (Jumapili) nisingeweza kupanda nalo kwa kuwa muda tuliopewa ni mfupi sana,” alisema Diamond.

Alipobanwa kuhusu kutumia jeneza la Kikristo na kuhusishwa na fununu za kubadili dini, alisema hana mpango huo kabisa.
“Naomba nieleweke, mimi sikuwa na nia tofauti zaidi ya kuwakilisha kilichopo katika wimbo wangu. Lengo lilikuwa kuonesha uhalisia tu wa kibao changu cha Nikifa Kesho, siyo zaidi ya hivyo,” alisema.
Inasemekana kwamba Diamond aliamua kubadilisha uamuzi wake wa kupanda na jeneza jukwaani siku hiyo baada ya kunyetishwa na watu wanaomtakia mema kuwa asingeonesha picha nzuri kwa jamii, hasa kwa vile jeneza hilo lilikuwa na msalaba juu ya mfuniko.

PICHA 50 ZA MATUKIO SIKU YA KUAGA MWILI WA MAREHEMU ISAAC SEPETU