Saturday 13 July 2013

KAULI YA MENGI JUU YA WAUZA MADAWA YA KULEVYA NCHINI


Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amesema ikiwa mafisadi hawatadhibitiwa, iko hatari wakajiimarisha kufikia hatua ya kuiongoza nchi siku zijazo.
 “Wala rushwa wakubwa ni kina nani na wako wangapi?  Ukiniuliza mimi nitakwambia hawazidi wanne, wanafahamika ila sitawataja kwa leo,” alibainisha.


Alisema rushwa kubwa ipo nchini na tuendako ana wasiwasi kuwa wala rushwa wakubwa ndiyo watatawala nchi kupitia matakwa yao  kwa nchi kuongozwa na kutawaliwa na watu wasioonekana wala kujulikana.
Ni watu wenye nguvu wanajipenyeza hadi katika vyombo vya dola, mtu anaweza kupoteza kazi kwa uamuzi wao,” alisema.
Dk. Mengi aliongeza kuwa wapo wanaosema tatizo la rushwa litamalizwa kwa utashi wa kisiasa, lakini hauwezi kufanikiwa kama hakuna utekelezaji na kutambua kuwa rushwa kubwa inateketeza Taifa.
Alisema kuna sababu nne zinazosababisha mafisadi wasishughulikiwe ikiwamo kuogopwa kwa kuwa wana nguvu za kuwadhuru wanaowashughulikia, mlolongo wa utoaji rushwa na kuna wanaonufaika na ndiyo wanaotakiwa kuwashughulikia na kukosekana kwa ujasiri wa kuwashughulikia.
Dk. Mengi alibainisha kuwa wala rushwa wakubwa hapa nchini wako wanne na wanafahamika lakini kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuogopwa, wameendelea kutafuna mali ya umma bila woga wowote.


Alisema ripoti ya hivi karibuni ya masuala ya rushwa iliyotolewa na Shirika la Transparence International, imeonyesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 14 kwa rushwa, hali ambayo inatisha.
Alisema matokeo ya rushwa ni mabaya kwa watu maskini kwani ni wizi wa kumwibia mvuja jasho.
Mengi alisema wapo wanaosema kuwa yeye (Mengi), si mwathirika wa rushwa lakini ukweli ni kwamba alipoteza miradi mikubwa miwili kutokana na kukataa kutoa rushwa.


Sitataja kuwa miradi yangu ilipotea katika awamu ipi ya serikali, lakini sijakata tamaa na sitaogopa nitaendelea kuzungumzia na kupambana na rushwa,” alisema.
Alisema haiwezekani kuendesha nchi kwa misingi ya rushwa, hivyo ifike mahali Taifa likubali kutengana nayo na kuwatenga wala rushwa wakubwa na wadogo, lakini kuendelea kuwakumbatia Taifa litaanguka.
Alisema Taifa linakabiliwa na tatizo la uwapo wa watu wasiofahamu kitu kujinadi kuwa ndiyo wanafahamu na kuhusika katika maamuzi ya kupanga kodi kwa wafanyabiashara.
Alisema kwa sasa anafanya sala Taifa lisifike mahali mafisadi kutawala na kuachwa wafanye watakavyo.
Aidha, alisema kuna uhusiano mkubwa kati ya wala rushwa wakubwa na mtandao wa biashara ya dawa za kulevya.
Alisema biashara ya dawa za kulevya inakua na vijana ndiyo wanatumika katika biashara hiyo.
Huwezi kutenganisha biashara ya dawa za kulevya na wala rushwa wakubwa, hawa  ndiyo wafanyabiashara wa dawa za kulevya, wanawatumia vijana kufanikisha biashara zao,” alisema.
 “Vijana na wasanii wetu wanatumika katika biashara hii, waliokamatwa Afrika Kusini si rahisi wawe na kiasi hicho cha fedha, bila ufadhili wa wala rushwa wakubwa, aliyewatuma si mtu mdogo bali mla rushwa mkubwa,” alisema Dk. Mengi.


Aidha, alisema vijana ndiyo tegemeo la Taifa na wateja wa bidhaa zinazouzwa na wafanyabiashara, hivyo upo wajibu mkubwa wa kupinga kwa vitendo suala la rushwa.
Alisema ni lazima Watanzania wachukue hatua za kukabiliana na wala rushwa na lawama kubwa ni kwa Watanzania ambao wanashindwa kuwaunga mkono  wanaopinga rushwa.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, Godfrey Simbeye, alisema ripoti iliyozinduliwa ilijikita katika kuangalia mazingira ya uwekezaji Tanzania na kubainisha mambo yanayokwamisha uendeshaji na ukuaji wa biashara nchini.
Alisema wengi wa wafanyabiashara waliohojiwa waliainisha vikwazo kuwa ni ukosefu wa umeme, kiwango cha kodi, rushwa na mrundikano wa kodi.

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako