Saturday 13 July 2013

RAMADHANI CHOMBO 'REDONDO' AREJESHWA SIMBA SC

Kiungo Ramadhani Suleiman Chombo ‘Redondo’ amerejeshwa kwenye kikosi cha Simba SC, baada ya kuomba radhi kufuatia kusimamishwa miezi mitatu iliyopita kwa utovu wa nidhamu.
Redondo alisimamishwa kwa pamoja na nyota wengine, mabeki akina Paul Ngalema, Juma Nyosso, kiungo Haruna Moshi ‘Boban’ na mshambuliaji Abdallah Juma ambao wametemwa moja kwa moja.
Redondo alisajiliwa na Simba SC kwa mara ya kwanza mwaka 2007 akitokea Ashanti United ya Dar es Salaam pia, lakini baada ya misimu miwili akahamia Azam FC ambako alifanya kazi hadi msimu huu aliporejea nyumbani
 SHABANI CHOMBO REDONDO AKIINGIA UWANJANI KUPIGA TIZI

Pamoja na kumrejesha Redondo, Simba SC itasajili beki mwingine wa kati kutoka nchi jirani, ambaye kwa sasa anaitumikia nchi yake katika mechi za kuwania kucheza Fainali za Ubingwa wa Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
Ujio wa beki huyo utafanya sasa mabeki wawili Waganda, Samuel Ssenkoom na Assumani Buyinzi wagombee nafasi moja ya kusajiliwa na klabu hiyo, wakati kiungo Mganda pia, Mussa Mudde ataachwa.
Mganda mwingine Moses Oloya ambaye ameahidi kuja Simba SC Agosti mwaka huu atakapomaliza Mkataba wake Vietnam, atakamilisha dadi ya wachezaji wa kigeni wa Wekundu wa Msimbazi- wengine wakiwa wakia kipa Mganda pia, Abbel Dhaira, mmojawapo kati ya Ssenkoom na Buyinzi, Mrundi Amisi Tambwe na huyo beki wa nchi jirani anayeitumikia nchi yake hivi sasa kwenye CHAN. 
Maana yake wachezaji wengine wawili waliokuja kufanya majaribio, Felix Cuipoi raia wa DRC aliyekuwa anacheza Cameroon na Kun James kutoka Kusini hawana tena nafasi ya kusajiliwa Simba SC. 
Kwa sasa, kikosi cha Simba SC kipo Kahama mkoani Shinyanga, ambako kitacheza mchezo mmoja wa kujipima nguvu na Kahama United kesho kwenye wa Manispaa wilayani humo.
Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ amesema kwamba baada ya mchezo huo wa Jumapili, timu itaelekea Musoma mkoani Mara kucheza mechi moja zaidi.
Amesema mjini Musoma watacheza na kombaini ya Musoma kwenye Uwanja wa Karume Jumatano, yaani Julai 17 na baada ya hapo timu itarejea Dar es Salaam.
URA ya Uganda inatarajiwa kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kucheza na Simba SC Julai 20, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Simba, kabla ya kwenda Kahama ilikwenda Katavi ambako ilicheza mechi mbili na kushinda zote, 3-1 dhidi ya Rhino FC ya Tabora na 2-1 dhidi ya kombaini ya Katavi kwenye Uwanja wa wazi wa Katavi mkoani humo. 
Simba SC, ambayo ilikuwa Katavi kwa mwaliko wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika mchezo wake wa kwanza, mabao yake yalifungwa na Edward Christopher mawili na moja Nahodha mpya, Nassor Masoud ‘Chollo’ na mchezo uliofuata mabao yalifungwa na Kun James mshambuliaji aliye katika majaribio kutoka Al Ahly Shandi ya Sudan Kusini na beki Mganda, Samuel Ssenkoom kutoka URA. 

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako