HUKU skendo ya kunaswa akiwa na madawa ya kulevya
ikiendelea kumtesa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, Video Queen maarufu
Bongo, Agnes Gerald ‘Masogange’ anatarajiwa kupandishwa kortini nchini Afrika
Kusini leo kujibu shitaka ambalo mwenyewe hajaliweka wazi, Ijumaa linakupasha.
Agnes Gerald ‘Masogange’. |
HISTORIA
Mwishoni mwa wiki iliyopita, habari ya mjini
ilikuwa Masogange kanaswa na madawa ya kulevya nchini Afrika Kusini.
Habari zilisambaa kwamba sanjari na Masogange,
mwingine aliyenaswa naye ni mdogo wake (mtoto wa mama yake mdogo Agnes) aitwaye
Melisa Edward.
Kwa mujibu wa habari hiyo ya mjini,
wawili hao walinaswa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oriver Tambo uliopo
Kempton Park siku ya Ijumaa wiki iliyopita wakitokea Tanzania wakiwa na ‘mzigo’
wa kilo nyingi aina ya ‘crystal methamphetamine’ wenye thamani ya shilingi za
Kitanzania bilioni 6.8!
Melisa Edward aliyekamatwa na Agnes |
GAZETI LA IJUMAA LAANZA KUSAKA UKWELI
Baada ya kunasa habari hiyo, Ijumaa liliingia
mzigoni kuusaka ukweli ambapo hata hivyo, madai hayo yalikuwa yakijifungafunga
sana.
Mtu mmoja wa karibu na Masogange alipoulizwa kuhusu
ukweli au uongo wa habari hiyo alikuwa na haya ya kusema:
“Ni kweli Agnes amekamatwa akiwa na
madawa ya kulevya kule Sauzi. Lakini si yenye thamani hiyo ya bilioni sita bali
ni milioni arobaini tu. Hata hivyo, ameachiwa kwa dhamana ila paspoti yake
imezuiliwa.
“Nadhani kuna mambo yanawekwa sawa
ikiwezekana atarudi nyumbani.”
JIJINI DAR, KAMANDA WA KUPAMBANA NA MADAWA YA
KULEVYA ANENA
Jumatatu iliyopita, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha
Kudhibiti Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa aliviambia vyombo vya
habari kuwa, Watanzania wawili walikamatwa nchini Afrika Kusini na mamlaka ya
mapato wakiwa na madawa ya kulevya kutoka Tanzania yenye thamani ya shilingi
bilioni 6.8.
Kamanda Nzowa aliwataja Watanzania hao kuwa ni
Agnes Gerald ambaye ana miaka 25 na Melisa Edward mwenye miaka 24. Alisema
wawili hao baada ya kukamatwa na chombo hicho walikabidhiwa kwa polisi ambapo
mahojiano yanaendelea.
Dawa za kulevya lakini siyo walizokamatwa nazo akina Agnes na Melisa |
Baada ya Kamanda Nzowa kuwataja kwa majina wawili
hao Jumatatu iliyopita, siku iliyofuata, Ijumaa lilipiga hodi kwenye ofisi za
kamanda huyo kwa lengo la kutaka kujua kama Agnes Gerald aliyemtaja jana yake
ni Masogage au majina yanafanana tu.
Kamanda huyo hakuwepo ofisini kwake asubuhi hiyo na
kwa mujibu wa wasaidizi wake, alikuwa kwenye kikao cha dharura kwenye Ofisi za
Polisi wa Kimataifa ‘Interpol’.
ALIPOPIGIWA SIMU
Ilibidi Ijumaa limsake kwa njia ya simu ya
kiganjani kwa mara kadhaa. Alipopokea akaulizwa kuhusu Agnes Gerald aliyemtaja
kama ni Masogange yule staa.
Kamanda Nzowa: “Eee, mimi siwezi kusema ni huyo,
ninachojua ni Agnes Gerald tu basi. Sasa kama ni Masogange mimi sifahamu
lolote.”
JUMANNE USIKU SIMU KUTOKA SAUZI
Mpaka hapo, timu nzima iliyokuwa ikifuatilia habari
hiyo haikuona ukweli wa Agnes Gerald kuwa ni Masogange na kwa vile siku zote
Global Publishers inasimamia utafiti kabla ya kuandika habari iliamua kuiweka
pembeni kwanza ili kuendelea kuichimba.
Saa 2:14 usiku wa siku hiyo, Ijumaa lilipokea simu
yenye kuashiria wito (code number) ni ya nje na kabla haijapokelewa, ilibainika
ni ya Afrika Kusini.
Ijumaa: Haloo.
Sauti: Haloo, mimi Masogange.
Ijumaa: Mambo Agnes, pole sana na mkasa
uliokupata bwana, pole sana.
Agnes: Kwanza naumizwa sana na maneno
ambayo watu wanazidi kuyaeneza sehemu mbalimbali bila kuwa na uhakika wowote,
mimi sikukamatwa kwa sababu ya madawa ya kulevya.
“Mkasa nilioupata siyo ambao watu
wanaueneza kwenye mitandao mbalimbali na katika vyombo ya habari.”
Ijumaa: Kwa hiyo madai ya kukutwa na
madawa ya kulevya si ya kweli?
Agnes: Kweli nilikamatwa huku kwa
matatizo f’lan ila siyo ishu ya madawa kama watu wanavyosambaza.
Ijumaa: Ni tatizo gani sasa?
Agnes: Unajua sipendi tena kuwapa watu
faida ila lilikuwa ni tatizo la kawaida, nilikamatwa na baada ya hapo nilitoka
na niko huru. Nasubiri tu kwenda mahakamani Ijumaa (leo) mara moja kisha
n’tarudi Bongo.
Ijumaa: Mh! Sasa Egg, mbona huku mpaka
viongozi wa polisi wamesema ni madawa?
Agnes: Hapana, siyo, ipo ishu ndogo tu.
Ijumaa: Haya pole sana kwa misukosuko.
Agnes: Asante sana, nitakuja huko siku
si nyingi.
Habari hii imeandikwa na Imelda Mtema,
Haruni Sanchawa na Musa Mateja.
SOURCE: www.xdeejayz.blogspot.com
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako