Monday 30 September 2013

MKUU WA WILAYA MBULU ATOA STAILI YA UONGOZI PITIA UPATE PICHA



Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, Anatory Choya, amesema kuwa aliwapigia magoti wananchi wa Kijiji cha Hydom, ili kuonyesha unyenyekevu kwa wananchi hao aliodai walionekana kujazwa maneno ya uchochezi na wanasiasa ili wavuruge amani .
Alisema kutokana fujo zilizofanywa na baadhi ya wananchi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika majuzi, kwa nafasi yake angeweza kuagiza hata Jeshi la Polisi kuwadhibiti watu, lakini misingi ya dini yake haimruhusu kumdhuru mtu zaidi ya kumwonyesha unyenyekevu.
Alisema hali hiyo ndiyo iliyomfanya kuamua kupiga magoti na kumshtakia Mungu.
“Mimi ni mkristo, unyenyekevu ndiyo nguzo pekee ya kuonyesha upendo na kudumisha amani. Ningeweza kuagiza polisi wawadhibiti, lakini sioni sababu kwa kuwa hiyo siyo misingi ya utawala. Ndiyo maana nikaona bora nitumie njia nyingine ya kumshirikisha Mungu mbele yao,”alisema Choya na kuongeza:
“Wanasiasa wamekuwa wakipandikiza chuki kwa wananchi kwa makusudi kwa lengo la kuvuruga amani lakini kwa kumweka Mungu mbele nina imani tutafanikiwa ili siku moja tusije tukaingia kwenye mkumbo wa Syria na Misri”
Choya alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na Mwananchi Jumapili, siku chache baada ya kitendo chake cha kupiga magoti mbele ya wananchi kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Haydom.
Mkuu huyo wa wilaya alidaiwa pia kuwalaani baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Haydom kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kumdharau na kutofuata maagizo yake, wakati yeye amewasaidia katika kutatua migogoro mbalimbali waliyokuwa nayo.
Tukio hilo la kusikitisha lilijitokeza baada ya wananchi wa kijiji hicho kupinga agizo la Choya, lililowataka kufanya uchaguzi wa kaimu mwenyekiti wa kijiji hicho, kabla ya kufanya uchaguzi mdogo, ambapo walipinga kwa kudai kuwa hakuna sheria hiyo.
Mmoja wa wananchi hao alilumbana na mkuu huyo wa wilaya ambapo Choya alijibu; “Nami nitarudi kwetu.” Naye Tikin akasema tena: “Unasema utarudi kwenu Biharamulo wakati hawakutaki kwani ulifukuzwa ubunge?”
Maneno hayo yalionyesha kumkwaza Choya ambapo alipiga magoti huku machozi yakimlenga na kumwomba Mungu afanye jambo kwa watu wa Haydom kwani wanamdharau kabla ya kujitokeza wazee watatu wa Haydom na kumwomba msamaha mkuu huyo wa wilaya.
                                               

RAIS KIKWETE, BARA LAKE AFRIKA NA NCHI YAKE TANZANIA!!

RAIS WA TANZANIA
NDANI ya taarifa hii Rais Kikwete kiongozi aliye ndani ya bara la Afrika ameongea kile ambacho kwa sasa bara la Afrika na nchi nyingi za Afrika si ya kati wala kusini kuwa na wakati mgumu kurudisha hali ya utulivu na upendo ndani ya nchi..

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mwenendo wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kuhusu Bara la Afrika na viongozi wake, unainyima Mahakama hiyo nafasi kubwa ya kuungwa mkono na Bara la Afrika.

Rais Kikwete pia amelaani vikali mashambulizi yanayoongezeka dhidi ya vikosi vya kimataifa vya kulinda amani katika nchi mbali mbali duniani wakiwamo walinda amani wa Tanzania.

Rais Kikwete alitoa msimamo huo wa Tanzania mwishoni mwa wiki wakati alipohutubia Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mwaka huu, kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.

Katika hotuba yake fupi na iliyowavutia wasikilizaji, Rais Kikwete alisema kuwa ni dhahiri kuanzishwa kwa ICC kutokana na Mkataba wa Rome kulikuwa ni hatua muhimu sana katika mfumo wa kimataifa wa kupambana na makosa ya jinai.

“Kwa hakika kuundwa kwa Mahakama hiyo kuliweka mfumo mzuri wa kuondokana na watu kutenda vitendo vya jinai na kuweza kuepukana na kuwajibika kwa vitendo hivyo na Mahakama hiyo ilianzishwa kwa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na Afrika.

Hata hivyo, muongo mmoja tu baada ya kuanzishwa kwa Mahakama hiyo, ni dhahiri kuwa mvutano umezuka kati ya ICC na Bara la Afrika. Sasa Mahakama hiyo inaonekana kama taasisi isiyojali maoni na msimamo wa Afrika, kwa mambo ambayo kwa maoni yangu, ni hofu halali ya Waafrika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

    “Bado Mahakama hiyo inaendelea kupuuza maombi ya mara kwa mara ya Umoja wa Afrika. Ni jambo la kutia huzuni kuwa maombi ya kubadilisha muda wa kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Naibu Rais William Ruto yalipuuzwa na hata hayakujibiwa kabisa.”

    Ameongeza Rais: “Tabia hii imekuwa ni hitilafu kubwa ambayo inaleta kikwazo kwa ICC kushindwa kutimiza wajibu wake wa kupambana na tabia ya watu wanaofanya makosa ya jinai kutokuchukuliwa hatua. Kwa hakika, kugangamara kwa ICC hata katika masuala yaliyo wazi, kumethibitika kuwa kunainyima Mahakama hiyo nafasi ya kuendelea kuungwa mkono Barani Afrika.”

    Rais Kikwete alisema pia kuwa Tanzania sasa imekuwa moja ya nchi ambazo zinashiriki zaidi katika shughuli za kimataifa za kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa. Tanzania ina zaidi ya walinda amani 2,500 katika Darfur, Sudan; Lebanon na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kuwa ni nchi ya sita katika Afrika na ya 12 duniani kwa kutoa walinzi wa amani duniani.

    “Kwa hakika tunaridhishwa na mchango wetu mdogo katika shughuli hii. Na tunajua kuwa wakati mwingine tunalipa gharama kubwa na maisha ya vijana wetu kwenye shughuli hizi kama ilivyotokea majuzi katika Darfur na DRC. Waliopoteza maisha yao ni mashujaa wa taifa letu ambao maisha yao hayakupotea bure.”

    Aliongeza Rais Kikwete: “Vifo vya walinda amani wetu ni ukumbusho wa kutosha wa hatari zinazowakabili walinda amani wote duniani. Ni jambo la kuudhi, kwamba vikundi vyenye silaha na waharibifu wa amani duniani wanaongeza mashambulizi hayo dhidi ya watumishi wa amani. Ni lazima tulaani mashambulizi haya kwa nguvu zetu zote kwa sababu hakuna  sababu yoyote ya kuhalalisha mashambulizi haya ya kinyama ambayo ni kosa la kimataifa la jinai chini ya Sheria za Kimataifa.”

    Alisisitiza: “Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo wajibu wake mkuu ni kulinda amani na usalama wa kimataifa lazima liwe mstari wa mbele katika kulaani vitendo hivyo vya kinyama na haraka tu vinapotokea.”

    Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi katika Marekani na Canada ameondoka New York usiku wa leo, Jumamosi, Septemba 28, 2013, kurejea nyumbani ambako atawasili Jumatatu mchana.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
29 Septemba, 2013

MSAANII AMBAYE PIA NI PRODUCER WA MUZIKI MACK MALICK (MACK 2B,SIMBA) AFARIKI DUNIA

  

Msanii wa Kizazi Kipya kutoka Block 41, Kikosi cha Mizinga KALAPINA (NABII KOKO), akizungumzia Msiba wa mwanamuziki ambaye pia ni Producer wa Mizuki wa Mac Malick, Mack 2b (SIMBA)

Sunday 29 September 2013

POMBE SI CHAI

                             Baada ya Kugonga vitu vya kutosha hili likawa ndio pozi, namna hiyo!

VITA YA MAPENZI

Mabinti  wawili  ambao  walikuwa  ni  marafiki wa  damu.Urafiki wao uliingia  dosari  baada  ya  mabinti  hao  kusalitiana  na  kuchukuliana  wapenzi....




Anayevuja  damu  usoni ni  binti  ambaye  amechanwa   nyembe  na Magreth  ( rafiki yake ) akimtuhumu  kutembea  na  mpenzi wake.

Saturday 28 September 2013

OFISI YA MWANASHERIA MKUU YAFUNGUA OFISI 23 MIKOANI

Wakili wa serikali Mkuu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Frederick Manyanda (kulia) akieleza kwa waandishi (hawapo pichani) mkakati wa kuhakikisha kuwa huduma ya usimamizi na utoaji wa haki inawafikia wananchi wote kwa karibu kwa kufungua ofisi zaidi Mikoani, Katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO)  Jijini Dar es Salaam,katikati ni Afisa Habari toka ofisi hiyo Bi. Asiatu Msuya na kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Bi. Georgina Misama.



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI


OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAFUNGUA OFISI  23 KATIKA MIKOA MBALIMBALI KUFANIKISHA MPANGO WA UTENGANISHWAJI WA SHUGHULI ZA UPELELEZI NA UENDESHAJI WA MASHTAKA NCHINI


Utangulizi
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imefanikiwa kufungua Ofisi 23 katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro (Moshi), Arusha, Mwanza, Kagera (Bukoba) Mara (Musoma), Shinyanga, Tabora, Singida, Iringa, Mbeya, Mtwara, Lindi, Dodoma, Rukwa (Sumbawanga),Ruvuma (Songea), Njombe, Manyara,Morogoro,Kigoma,Geita  na Pwani. Aidha jumla ya Ofisi mbili (2) za zimefunguliwa katika Wilaya za Temeke na Monduli. Kwa mwaka wa fedha 2012/2013 pekee jumla ya Ofisi tano (5) zimefunguliwa katika mikoa ya Pwani, Kigoma, Morogoro, Manyara, Njombe na Geita ikiwemo pia Ofisi mbili za Wilaya.

Lengo
Lengo kuanzishwa na kuimarishwa kwa Ofisi hizi za Mikoa na Wilaya ni kuhakikisha kuwa huduma ya usimamizi na utoaji wa haki inawafikia wananchi wote kwa karibu zaidi. Baadhi ya huduma zinazotolewa ni pamoja na kuendesha Mashtaka mahakamani, kushughulikia malalamiko na kero za wananchi kuhusiana na kesi za jinai na madai zinazowakabili, kutembelea mahabusu na kuratibu upelelezi wa kazi za upelelezi wa makosa ya jinai zinazofanywa na vyombo pelelezi/chunguzi ikiwemo Polisi, Magereza, Uhamiaji,TAKUKURU.

Utekelezaji wa Mpango wa kutenganisha Upelelezi na Mashtaka nchini
Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kutekeleza mpango huu wa Utenganishwaji wa Upelelezi na Mashtaka kwa mujibu wa Sheria ambapo mfumo wa Sheria ambao uliwezesha kutungwa kwa Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, 2005 na Sheria ya Usimamizi wa Uendeshaji Mashtaka nchini, 2008 umeboreshwa; pamoja na kuanzishwa kwa Jukwaa la Ki-taifa la Haki-Jinai (National Criminal Justice Forum) Desemba 2009 linaloviunganisha pamoja vyombo vyote vinavyosimamia utolewaji wa Haki-Jinai nchini;

Serikali pia imeboresha  Muundo wa Divisheni ya Mashtaka kwa kuweka Sehemu (Section) mahsusi inayosimamia utekelezaji wa mchakato wa utenganishaji wa kazi za upelelezi na Mashtaka na uratibu wa kazi za ki-pelelezi; pamoja na kuanzishwa kwa huduma ya Mashtaka ya moja kwa moja ambako Mawakili wa Serikali wanaendesha kesi;  Hii imepelekea idadi ya kesi zinazofunguliwa Mahakamani ambako Mawakili wa Serikali wanaendesha Mashtaka kupungua ikilinganishwa na kipindi cha nyuma; Kuongezeka kwa ubora wa huduma zitolewazo na kupungua kwa kesi za kubambikizwa.

Utekelezaji wa Programu ya Utenganishwaji wa Mashtaka na Upelelezi (Civilianization) imetoa msukumo mkubwa kwa Ofisi kuingia uanachama na makubaliano ya mashirikiano na vyama vinavyohusiana na kazi za Uendeshaji Mashtaka duniani, kama vile-IAP, HOPAC, APA, EAAP, na ARINSA; Serikali itaendelea kupanua wigo wa uendeshaji wa Mashtaka kwa kuanzisha na kuimarisha Ofisi katika Wilaya zote nchini pamoja na Mikoa miwili iliyobaki ya Katavi na Simiyu.

Tunapenda kuwakumbusha Wadau wetu wote na Wananchi kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za uhalifu au jinai yoyote katika jamii kwa vyombo husika kupitia utaratibu unaofaa; na kutoa ushahidi Mahakamani pale unapohitajika kwa kuwa hizi  ni nguzo muhimu katika uendeshaji wa kesi mbalimbali. Aidha tunatoa wito kwa umma, wadau wetu na wananchi wote kwa ujumla pamoja na vyombo vya habari nchini kufuatilia mtiririko, hoja zinazowalishwa Mahakamani na uamuzi uliotolewa na Mahakama katika kesi mbalimbali zinazoendelea kuwa na taarifa sahihi ya kuhusu kesi hizo.

Imetolewa Na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Ijumaa, Septemba 27, 2013

 Kwa mawasiliano zaidi

OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
SLP 9050
KIVUKONI FRONT
DAR ES SALAAM
SIMU: +255 22 21181778
NUKUSHI: +255 22 2113236
BARUA PEPE: info@agctz.go.tz 
TOVUTI:            www.agctz.go.tz