Monday 23 October 2017

ZIARA YA NAIBU WAZIRI SHONZA

NAIBU WAZIRI WA HABARI JULIANA SHONZA KUSHOTO AKIPATA MAELEKEZO KUTOKA KWA VIONGOZI WA TBC


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza amewaasa wanahabari kutumia vizuri taaluma yao katika kutoa habari zenye weledi zinazoleta manufaa kwenye jamii na kusisitiza kuwa endapo taaluma hiyo ikitumika vibaya inaweza kusababisha madhara makubwa sana kwa jamii.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika makao makuu ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) barabara ya TAZARA jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Shonza amesisitiza ushirikiano kati ya serikali na wanahabari ili kuipeleka mbele zaidi taaluma ya habari nchini.
Vile vile Naibu Waziri Shonza ameipongeza TBC kwa kuwaamini vijana na kuwapa fursa kubwa ya kufanya kazi na kuendana bega kwa bega na sera ya serikali inayosisitiza kutoa nafasi nyingi kwa vijana katika kulitumikia taifa.
Amesema anashukuru sana kwa ushirikiano aliopewa na TBC na kusisitiza kuwa kwa kushirikiana na Waziri Mwenye dhamana ya wizara hiyo wanashughulikia changamoto zote zinazolikabili shirika hilo.
Ameipongeza TBC kwa kuwa mfano bora miongoni mwa vyombo vingi vya habari nchini na kuviasa vyombo vingine kufuata misingi bora ya taaluma ya habari.
NAIBU WAZIRI AKIWA NDANI YA STUDIO ZA TBC INTERNATIONAL
Hii ni ziara ya kwanza kwa Naibu Waziri Shonza kufika TBC tangu alipoteuliwa na Rais Dkt. John Magufuli Oktoba saba mwaka huu akichukua nafasi ya Anastazia Wambura.
NAIBU WAZIRI SHONZA ALIPOTEMBELEA STUDIO ZA TBC FM
Habari/picha
Hamisi Hollela na Mahmud Rajab