SIKU chache baada ya kukamatwa kwa askari 'feki' wa Usalama
Barabarani mwenye cheo cha Sajini, akifanya kazi ya kuongoza magari eneo ya
Tabata Kinyerezi, Dar es Salaam, mambo mapya yamezidi kubainika juu ya sababu
za mtu huyo kujiingiza katika kazi hiyo bila kutambuliwa na Jeshi la Polisi.
Habari zilizotufikia kutoka
vyanzo vya kuaminika, zinasema trafiki huyo 'feki', ambaye inadaiwa jina lake halisi
ni James Juma Hussein (45), mkazi wa Kimara Matangini, alianzia kazi hiyo
mkoani Singida kabla ya kujipa uhamisho wa kikazi kwenda Dar es Salaam.
Chanzo chetu kilieleza kuwa, trafiki huyo alikuwa
na shemeji yake aliyeitwa Shaban ambaye aliajiriwa na Jeshi la Polisi Kitengo
cha Usalama Barabarani aliyekuwa akifanyia kazi mkoani Tabora.Vyanzo vyetu
viliongeza kuwa, baada ya shemeji yake kufariki mkoani Tabora, trafiki huyo
alipata mwanya wa kuchukua nguo za kazini alizokuwa akizitumia shemeji yake.
Inadaiwa trafiki huyo 'feki', aliwahi kupata
mafunzo ya upolisi katika Chuo cha Polisi Moshi (CCP), mkoani Kilimanjaro
lakini alifukuzwa.Chanzo hicho kiliongeza kuwa, baada ya ndugu wa trafiki huyo
kufariki dunia, trafiki 'feki', alikuwa akifanya kazi hiyo bila ndugu zake
kujua akianzia mkoani Singida bila kushtukiwa.
"Jamaa aliamua kujirithisha kazi ya shemeji yake, alikwenda
Singida na kufanya kazi hiyo kwa muda usiojulikana," kilisema chanzo
chetu.Chanzo hicho kiliongeza kuwa, kutokana na uchache wa matrafiki mkoani
Singida, aliingiwa hofu ya kuweza kujulikana; hivyo aliamua kujipa uhamisho wa
kwenda jijini Dar es Salaam.
"Akiwa Dar es Salaam, alifanya kazi hii kwa muda mrefu bila
kujulikana hadi alipokamatwa wiki iliyopita akiwa eneo lake la kazi akiongoza
magari," kilisema chanzo hicho.Mtoa habari huyo alisema polisi walianza
kumtilia shaka trafiki huyo kutokana na adhabu zake alizokuwa akizitoa kwa
madereva.
"Tulianza kuwa na hofu naye kwa sababu yeye adhabu zake kwa
kila dereva aliyekuwa akimkamata alimtoza sh. 20,000 hadi 25,000,"
kilieleza chanzo hicho.Sababu nyingine iliyowafanya polisi wamtilie shaka ni
utamaduni wake wa kuondoka mapema kwenye kituo cha kazi ambavyo alikuwa
akijipangia mwenyewe.
"Trafiki akiwa kazini, inabidi awe kituoni kwake kuanzia
asubuhi hadi jioni muda wa kazi unapomalizika, tulishangaa kuona mwenzetu
anaingia kazini asubuhi na kuondoka kabla ya muda wa kazi," kiliongeza
chanzo hicho.Inadaiwa trafiki huyo alikuwa akifanya hivyo baada ya kukamilisha
mahesabu yake aliyokuwa amejiwekea ambapo hali hiyo iliwafanya polisi waanze
kujiuliza maswali na ndipo walipoanza kumfuatilia.
Baada ya kufuatiliwa bila yeye kujua, walibaini hata upigaji wake
wa saluti ni utata mtupu ambapo kutokana na hali hiyo, waliweka mtego na kufanikiwa
kumkamata.
Hadi sasa anaendelea kushikiliwa na Jeshi la
Polisi ambalo limeahidi kutoa taarifa kamili baada ya uchunguzi wao kukamilika
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako