MPTO AKIWA AMEKULA POZI NDANI KWAKE....JE UNAPAONAJE |
Utunzi wa
Mashairi, mikogo na staili yake ya mavazi jukwaani inaweza kuwa chanzo cha
kumfanya aonekane mfano wa simba dume la Afrika linalong’ara anga za kimataifa
kutoka hapa nchini.
Ni baadhi ya
sifa zinazombeba msanii Mrisho Mpoto maarufu kama ‘Mjomba’, ambaye kwa asili ni
Mngoni kutoka Kijiji cha Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mpoto a.k.a
Mjomba anaweza kuwa mmoja kati ya wasanii wachache barani Afrika wanaofanya
vizuri katika muziki wa asili unaonogeshwa na ghani za mashairi sanjari na
ushereheshaji katika kuwasilisha ujumbe jukwaani.
Alitambulika
rasmi katika sanaa kupitia kibao chake cha Salamu Zangu na kuzidi kuonyesha
zaidi uwezo wake katika sanaa alipotoa nyimbo za Adela, Mjomba, Chocheeni Kuni
na nyinginezo, ingawa alianza kujulikana katika mataifa makubwa yakiwemo
Uingereza, Marekani, Uholanzi na Ufaransa.
Hata hivyo,
kwa maelezo yake Mjomba anasema kuwa safari ya maisha yake ilikuwa na
changamoto nyingi hadi kufikia mafanikio aliyonayo sasa akimtaja kaka yake kuwa
mtu wa kwanza kumkatisha tamaa katika safari yake aliyekuwa akiishi Kigoma.
“Mwaka 1995
‘braza’ aliniita Kigoma akaniambia niachane na sanaa hii, akanitafutia vibarua
vya kubeba mizigo pale Bandari ya Kigoma, baada hapo nikabobea na hatimaye
nikaingia kwenye ajira ya uvuvi wa samaki,” anasema.
Anaongeza
kuwa alifanya kazi hiyo kwa miaka miwili, lakini kabla ya hapo alikuwa akiishi
na mama yake jijini Dar es Salaam kuanzia mwanzoni ya miaka ya 1990.
Anadokeza
kuwa kipindi hicho alikuwa na hali ngumu akiishi kwa kufanya vibarua ili kupata
riziki ya kila siku.
“Mama alikuwa akifanya kibarua cha kubangua dengu na korosho
katika Kampuni ya ‘Mohamed Enterprises’, kwa hivyo nilikuwa naongozana naye
kila siku,” anasema
Pamoja na kuwepo kwa wasanii wa Bongo
Fleva wenye thamani za juu, Mpoto anaweza kuwa mmoja wa wasanii wenye kipato
cha juu kutokana na kipato chake anachokipata kwa mwezi kupitia sanaa.
Pia ni
mjasiriamali anayemiliki mabasi matatu ya (Daladala) yanayomwezesha kukusanya
hadi Sh300,000 kila siku. Upande mwingine katika sanaa amefanikiwa jipenyeza katika
soko na kupata mialiko mbalimbali kutoka taasisi, wizara, asasi na mashirika
inayomwingizia wastani wa Sh75 milioni kwa mwezi.
“Kwa mwezi
napata mialiko isiyopungua 15, kila mwaliko malipo hayapungui Sh5 milioni,
hivyo ukipiga hesabu mwenyewe utajua,” Mpoto anaweka wazi.
Hata hivyo,
anasema kuwa maonyesho ya hapa nchini hayamlipi kama ilivyo kwa mialiko na
maonyesho anayopata na kufanya nje ya nchi.
“Kwa mfano
mwaka huu nimekwenda Uingereza, Marekani, Burundi na Kenya. Kwa mialiko ya nje
napata posho ya kujikimu Paundi 120 kwa siku na malipo ya wastani wa Paundi
1500 mpaka 3000 kwa kila shoo,” anasema.
Fedha hizo
ni sawa na wastani wa Sh288,000 kama posho ya kujikimu na Sh3,600,000 hadi
Sh7,200,000.
Alikotokea
Mrisho Mpoto
ni moja ya vipaji vilivyoibuliwa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam(UDSM).
Anaeleza
kuwa yeye aliibuliwa kupitia mfumo wa awali wa chuo kutafuta vipaji mbalimbali
vya sanaa kwa ajili ya kuunda kikundi cha sanaa kilichopo chuoni hapo.
“Nilianza
kuishi chuoni hapo tangu mwaka 1993, nilikuwa nakula, nalala na kuishi kama
mwanafunzi pale huku nikishiriki mafunzo ya sanaa kupitia umoja wa Wanachuo
DARUSO,” anasema.
MPOTO AKIWA KATIKA TABASAMU ZITO |
Alifanikiwa
kukaa chuoni hapo kwa kipindi cha takriban miaka kumi kabla ya kuwa mmoja wa
waanzilishi wa Kikundi cha Parapanda, mnamo mwaka 1994. Hata hivyo hakuweza
kufanya shoo zake binafsi tofauti na mialiko ya chuoni kutokana na mwongozo wa
Kikundi cha DARUSO.
Anaongeza kuwa kipindi hicho pia alifanikiwa kuishi Ulaya na
Marekani kwa miaka kadhaa kutokana na sanaa yake.
“Lakini pia mwaka 2000 mpaka 2002
nilipata nafasi ya kusoma kozi ya mafunzo ya ‘Theatre’ nchini Marekani,
nilikuwa situlii hapa Tanzania hadi nilipokuja kutoa nyimbo ya Salamu Zangu,”
anasema.
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako