Saturday 3 August 2013

KING MAJUTO AVUTA JIKO



Kuna taarifa kwamba gwiji la sanaa za vichekesho nchini, Amri Athumani ‘King Majuto’ almaarufu kama mzee Majuto amefunga ndoa ya siri ndani ya Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani
Inasemekana kuwa tukio hilo limetokea Julai 8, mwaka huu pande za Mbagala Zakhem jijini Dar ambapo mzee Majuto alifunga ndoa na msichana aitwaye Rehema Omary.
Mzee Majuto aliambatana na wasanii wenzake Suleiman Barafu aliyekuwa mpambe wake na mwingine aliyefahamika kwa jina la utani kama mama Sharon.
Baada ya waandishi kupata taarifa kuhusu tukio hilo, waliwahi kutia timu Mbagala, nyumbani kwa binti huyo.
Baada ya kufika, ilibainika kuwa ni kweli kulikuwa na shamrashamra za ndoa ambayo ilikuwa ikifanyika kwa siri huku watu wakizuiliwa kupiga picha.
Muda mfupi baadaye, gari aina ya Toyota Noah lililowabeba mzee Majuto na wapambe wake liliwasili.
Muoaji akaongozana na wakwe na mashehe kwenda Msikiti wa Aqswa uliopo jirani ambapo ndoa hiyo ilifungwa kisha wakarudi nyumbani ambako cherekochereko ziliendelea.
Baada ya robo saa, mzee Majuto na mkewe walitoka ndani ya nyumba hiyo na kuingia kwenye gari hilo aina ya Noah.
Baada ya tukio hilo, mwandishi wetu alijaribu kuzungumza na mzee Majuto kwa simu lakini kazi haikuwa nyepesi kwani simu yake ilikuwa ikiita bila ya kupokelewa.
Alilipopigiwa simu mpambe wa bwana harusi, Barafu, alisema hana la kusema na kusisitiza atafutwe mzee Majuto.
Mwandishi alirudi Mbagala kwa mama wa biharusi ambaye alikuwa mkali na kusema kuwa atafutwe mzee Majuto.
Siku hiyohiyo mzee Majuto alipokea simu na kuulizwa kama ni kweli amefunga ndoa na msichana aitwaye Rehema.
Katika hali ya kushangaza, mzee Majuto alicheka sana na kudai kwamba utafiti wake umekamilika. Alipohojiwa ni utafiti gani alisema:
“Nilikuwa nafanya utafiti wa kutaka kuigiza filamu ya ndoa ya siri ndiyo maana nikaenda kule Mbagala lakini sasa nimeamini kwamba hakuna ndoa ya siri,” alisema mzee huyo huku akikwepa kukubali.
Habari zinasema kwamba mzee Majuto anakwepa kukubali kwamba amefunga ndoa kwa kumhofia mkewe wa kwanza ambaye amemuacha jijini Tanga.

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako