Thursday 15 August 2013

KIBANDA NA KESI YA KUJIBU

ALIYEKUWA MHARIRI WA TANZANIA DAIMA ABSALOM KIBANDA


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuona aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi, kuwa wana kesi ya kujibu.
Hakimu Mkazi Waliarwande Lema, alitoa uamuzi huo jana baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi wa mashahidi watatu.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuandika na kuruhusu kuchapisha makala ya uchochezi, inayodaiwa kuwahamasisha askari wa majeshi mbalimbali nchini, kutotii amri ya wakuu wao.
Mbali na Kibanda washitakiwa wengine ni mwandishi wa makala hiyo iliyochapishwa Novemba 30, mwaka juzi, Samson Mwigamba na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi, Theophil Makunga.
Baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi, wakili wa Upande wa Utetezi, Isaya Matambo, aliomba Mahakama iwape Mwenendo wa Kesi ili waandae majumuisho ya hoja kuwa washitakiwa hawana kesi ya kujibu, hata hivyo Hakimu Lema alikataa kutoa nafasi hiyo.
Alisema baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, ameona washitakiwa wana kesi ya kujibu na watatakiwa kuanza kujitetea Septemba 3 mwaka huu.
Aidha alisema atatoa hati ya kukamatwa kwa Mwigamba, endapo hatawasilisha vilelezo kuthibitisha sababu za kutofika mahakamani alizotoa kwamba anaumwa.
Alitoa onyo hilo baada ya mdhamini wa Mwigamba, Rose Moshi kudai mshitakiwa hajafika mahakamani kwa kuwa anaumwa na amelazwa katika Hospitali ya St Thomas Arusha.
Kibanda na Mwigamba wanadaiwa kuchapisha makala hayo, Makunga anadaiwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi, aliruhusu kampuni yake kuchapisha gazeti la Tanzania Daima, likiwa na makala hiyo inayodaiwa kuwa ya uchochezi.
Gazeti hilo lilikuwa na makala iliyokuwa na kichwa cha habari “Waraka maalumu kwa askari wote, iliyoandikwa na Mwandishi wa Safu ya Kalamu ya Mwigamba, Samson Mwigamba.

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako