Sunday 11 August 2013

UKWELI JUU YA SUALA LA POLISI KUMPIGA RISASI SHEHE PONDA MOROGORO

TUKIO la polisi kupiga risasi na kumjeruhi Shekhe Ponda Issa Ponda mjini Morogoro ni utata mtupu wakati baadhi ya waumini wa kiislam wa mjini humo wakithibitisha taarifa hizo kwamba Shekh Ponda kapigwa risasi begani, jeshi la Polisi mkoani humo limekanusha taarifa hizo, japo linalikiri walitaka kumkamata jioni hii waliposkia yupo kwenye mkutano wa hadhara.
Kamanda wa Polisi wa mkoani humo, Faustine Shilogile, amenukuliwa hivi punde na Radio One Stereo na kudai jeshi lake lilikuwa likimvizia kumkamata Sheikh Ponda baada ya kuhudhuria Kongamano la Wahadhiri wa Kiislam mkoani Morogoro na kuhutubia, lakini wakazidiwa ujanja na waumini waliomkinga na kumtorosha Shekh wao huyo machachari asiishie mikononi mwa dola.
Kamanda Shilogile, alisema suala la Ponda kupigwa risasi na kujeruhiwa au kuuwawa kama habari hizo zilivyozagaa mjini humo ni uzushi kwa vile shekh huyo hajafikishwa kituo chochote cha polisi au hospitali kama ni kweli kajeruhiwa.

 "Hizi ni habari zilizozagaa mjini hapa wengine wakidai ameuwawa, ila ukweli ni kwamba Polisi hawajafanya kitendo chochote dhidi ya Ponda zaidi ya kwamba tulitaka kumkamata mara baada ya kuhutubia kwa dakika kama 5 kwa kutambua kuwa anasakwa," alisema Shilogile; wakati wanamvizia Sheikh Ponda aliyechelewa kwenye kongamano hilo likiwa kama dakika 10 limalizike waumini wa kiislam aliodai walikuwa wengi mno walimtorosha na hivyo wao kumkosa na kudai kuwa wanafuatilia mahali alipofichwa na kama ni kweli alijeruhiwa wajue anatibiwa wapi.
Utata unakuja wakati Shilogile akisema hawakufanya tukio lolote la kupiga risasi, je wanafuatilia mahali anapotibiwa kwa sababu zipi? Kadhalika waumini waliozungumza kwa njia ya simu wamedai tukio hilo limetokea wakati Polisi walipovamia taksi iliyomleta Shekh Ponda na katika purukushani walifyatua mabomu ya machozi na risasi za moto ambapo ilimpata begani na kumjeruhi.
"Hawa watu wanatuchokoza Waislam ili tuonekane wakorofi tunasherehekea sikukuu yetu kwa amani wanatuletea mambo ya kihuni walitaka kumkamata Sheikh wetu nasi tukasimamia kidete na kuwagomea ndipo wakaamua kutumia nguvu kupiga risasi na kwa bahati ikampiga risasi ya bega na kumjeruhi wanakanusha nini," alisema mmoja wa mashuhuda hao.



No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako