Dar es Salaam. Klabu 13 za Ligi Kuu Bara, zimeitosa Yanga njiani baada ya kupitisha azimio la pamoja kukubali udhamini wa Kampuni ya Azam Media. Klabu hiyo ya Jangwani, sasa inabaki pekee kupinga udhamini wa Azam.
Hivi karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupitia Bodi ya Ligi (TPL) na Kampuni ya Azam waliingia mkataba wa Sh168 milioni kuonyesha mechi zote za Ligi Kuu kupitia kituo cha Azam TV.
Katika udhamini wa klabu, kila timu itapata kiasi cha Sh100 milioni kama haki ya kurushwa ‘live’ mechi zao za Ligi Kuu nyumbani na ugenini.
Wakizungumza jana Dar es Salaam, viongozi wa klabu za Simba, Azam, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Ashanti United, Rhino Rangers, Mbeya City, Prisons, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Costal Union, Mgambo JKT na JKT Oljoro kwa kauli moja walikubali mkataba wa Azam.
Walisema wanaamini udhamini huo utazisaidia klabu kujiimarisha kiuchumi na kuondoa kilio cha muda mrefu cha ukosefu wa wadhamini kilichozitesa klabu nyingi.
“Tumeona vizuri kutoa msimamo wa pamoja. Ukweli ni kwamba, hatuungani na Yanga kukataa udhamini huu ambao una masilahi kwetu,” walisema viongozi hao.
“Kilio chetu ni wadhamini na kwa bahati nzuri kuna dalili ya mambo kwenda vizuri. Tunawashangaa wenzetu wa Yanga kuwa kutounga mkono mkataba huu,” alisema Ezekiel Kamwaga (Msemaji wa Simba) kwa niaba ya viongozi wengine wa klabu.
Kamwaga alisema hakuna nchi zilizo jirani na Tanzania ambako timu zina mkataba mnono kama ilivyo kwa klabu zinazocheza Ligi Kuu
Naye Mwenyekiti wa klabu ya Mtibwa Sugar, Hamed Yahya na ambaye pia ni Mjumbe wa PTL alisema kuwa hoja zote zinazotolewa na Yanga juu ya suala hilo hazina mashiko kwani walishirikishwa mwanzo wa mchakato mpaka mwisho. Kuna taarifa kuwa Yanga iligomea udhamini wa Azam baada ya kupata udhamini wa Kampuni ya Vinywaji ya Pepsi ambayo ipo tayari kutoa kiasi cha Sh600 milioni.
Wakati huohuo, Yanga jana imeichapa Mtibwa Sugar mabao 3-1 katika mechi ya kirafiki iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mabao ya Yanga yalifungwa na Said Bahanuzi (26), Jerry Tegete (81) na Hussein Javu (87), wakati bao la Mtibwa lilifungwa na Shaaban Kisiga (58).
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako