Katibu wa taasisi na Jumuiya
za Kiislam Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda mkazi wa Dar es salaam jana asubuhi
amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Morogoro kwa
usafiri wa helkopta ya jeshi la polisi kujibu shitaka linalomkabili.
Ponda alifikishwa mahakamani hapo
chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi wakiwa na mbwa baada ya kuwasili
kwa helkopta hiyo iliyotua majira ya saa tatu subuhi katika uwanja wa Gofu
mjini Morogoro ikitokea jijini Dar es salaam.
Wakili wa Serikali, Bernard Kongola
alisoma mashitaka matatu dhidi ya Sheikh Ponda mbele ya hakimu mkazi
Mfawidhi mkoa wa Morogoro Richard Kabate alisema, mnamo Agosti 10 mwaka huu
katika eneo la Kiwanja cha Ndege manispaa ya Morogoro Ponda
aliuambia umati wa watu uliokusanyika kwenye mkutano wa hadhaza “ndugu waislamu
msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani kamati hizo
zimeundwa na Bakwata ambao ni vibaraka wa CCM na serikali na kama watajitokeza
kwenu watu hao na watajitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za
misikiti, fungeni milango na madirisha ya msikiti yenu na muwapige sana”
Kongola aliimbia mahakama hiyo kuwa
kauli hiyo iliumiza imani za watu wengine na kwamba hatua hiyo ni kinyume cha
agizo la mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Dar-es-salaam iliyotolewa
na hakimu V. Nongwa, Mei 9 mwaka huu ambayo ilimtaka Ponda ndani ya
kipindi hicho cha mwaka mmoja kutohubiri mambo ya uchochezi ambayo ni kinyume
na kifungu cha sheria namba 124 cha mwaka 2002, shitaka ambalo alikana.
Katika shitaka la Pili, Ponda
alidaiwa, Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege manispaa ya
Morogoro na mkoa wa Morogoro aliwaambia waislam serikali ilipeleka jeshi Mtwara
kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa
kuwaua, kuwabaka, na kuwatesa
wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni waislamu lakini serikali
haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa mwarabu asipatiwe kipande
cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya
wakazi wake ni wakristo na kusema maneno hayo yaliumiza imani
za watu wengine ambapo ni kinyume cha kifungu cha sheria 129 cha mwaka
2002 shitaka ambalo pia Ponda alikana.
Kwa upande wa utetezi, Ponda alikuwa
akitetetewa na wakili Ignas Pungu na Bantalomeo Tarimo, huku upande wa serikali
walikuwa wanaongozwa na Benedict Kongola, Gloria Rwakibalila, Asnab Mhando
Shekhe Ponda Issa Ponda
aliwasilishwa kwa helkopta ya jeshi la polisi katika uwanja wa Gofu mjini
morogoro akiwa chini ya ulinzi wa polisi na kupandishwa katika gari maalum
ambalo liliongozana na magari mengine matatu ya polisi huku ulinzi ukiwa
umeimalishwa katika eneo la mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro wakiwemo
askari wa Kikosi cha Kutuliza ghasia, wa upelelezi usalama wa taifa
pamoja na mbwa wa jeshi la polisi wakati shughuli za kazi katika mahamaka hiyo
na ofisi za jirani zikiwa zimesimama kwa muda.
Alifikishwa uwanja wa mahakama
majira ya saa 5.00 kamili asubuhi magari yalisimama kwa takribani dakika
30 ndipo askari walishuka kwenye gari na kumfungulia mlango kisha kushuka na
kuongozwa kwenye mahakama ya wazi ya hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa
Morogoro huku umati wa wananchi ukiwa umefurika mahakamani hapo na kushuhudia
kilichokuwa kinaendelea.
Baada ya Kusomwa kwa mashtaka yote
matatu wakili wa serikali aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi umekamilika
na kupanga kesi kuanza kusikilizwa septemba 2 mwaka huu ambapo kwa upande wa
utetezi uliomba mahakama kupanga kuanza kusikilizwa kwa kesi agosti 26 mwaka
huu hali ambayo ilimlazimu hakimu Kabate kuwapa muda wa kujadiliana ambapo
walitumia dakika tano kujadiliana na kurejea mahakamani na kupanga kuanza
kusikilizwa kesi agosti 28 mwaka huu.
Mawakili wa upande wa utetezi
walisema sababu za kuomba terehe hiyo ya kusikilizwa kwa kesi kwa kile
walichoeleza kuwa mteja wao bado ni mgonjwa na anahitaji kupatiwa matibabu ya
mara kwa mara hivyo anahitaji uangalizi.
Hata hivyo mahakama ilipomalizika
hali ya ulinzi iliendelea kuimarishwa na kupandishwa kwenye gari maalum
alilopanda na kuelekea kwenye uwanja wa Gymkana majira ya saa sita mchana
na kupandishwa kwenye helkopta kwa ajili ya kurejeshwa gerezani jijini
Dar-es-salaam.
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako