STAA wa muziki
wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ ambaye hakaukiwi na stori, safari hii
amekuja na mpya baada ya kuibuka na jeneza lenye msalaba ambalo limeibua
maswali mazito, Risasi Mchanganyiko linakupasha.
Diamond ambaye wimbo wake mpya wa ‘Number One’ upo katika chati ya
juu katika muziki huo, usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita aliingia na jeneza
hilo katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar na kusababisha maswali
mengi tata kutoka kwa mashabiki waliojazana kwenye onesho la Serengeti Fiesta
2013.
ILIKUWA SAPRAIZI
Mapaparazi wa
Risasi Mchanganyiko waliokuwa wamejaa katika viwanja hivyo wakihakikisha
wananasa matukio muhimu hasa yale ‘exclusive’, walipenyezewa mapema kuhusu
Diamond kuingia na jeneza.
Mtoa habari alisema Diamond aliingiza jeneza viwanjani humo kwa
lengo la kupanda nalo jukwaani wakati akiimba wimbo wake uitwao Nikifa Kesho
ambao mashabiki wake wengi wanasema amejichulia kifo.
Kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini, mtoa habari huyo
ambaye ni mtu wa karibu na Diamond alisema:
“Diamond
amekuja na jeneza, limefichwa kule nyuma wanakobadilishia nguo wasanii,
atapanda nalo jukwaani. Anataka kuwafanyia sapraizi mashabiki wake.”
SAPRAIZI YAKWAMA
Hata hivyo, baada ya matatizo ya kiufundi yaliyojitokeza, Diamond
hakuweza kupanda jukwaani Jumamosi usiku huo na badala yake akatakiwa kupanda
kesho yake Jumapili ambapo pia hakulitumia jeneza hilo kama mawazo yake ya
awali yalivyokuwa.
Mapaparazi wetu walisaka sehemu lilipohifadhiwa jeneza hilo na
kufanikiwa ambapo pia walikuta baadhi ya watu wakilishangaa na kuulizana
maswali.
MASWALI TATA
Nurdin Ali, mkazi wa Mbagala, Dar aliyeliona jeneza la Diamond
alisema:
“Mimi namkubali sana huyu bwana mdogo lakini sasa mambo ya
majeneza jukwaani ya nini tena?
“Sikubaliani na hili suala. Hata wimbo wake wa Nikifa Kesho sioni
kama una mantiki. Ni kama tu anajitabiria kifo. Anapita mlemle alimopita
marehemu Kanumba, maana naye aliimba wimbo akielezea itakavyokuwa siku akifa,
ikawa kweli.
“Lakini Diamond
amekwenda mbele zaidi kwa kuamua kuja na jeneza kabisa stejini. Sijui amenunua
au amekodisha, ila sikubaliani naye hata kidogo.”
MATUMIZI YA JENEZA
Mwingine aliyekataa kuandikwa jina lake gazetini alisema:
“Halafu kama lengo lake lilikuwa kuonesha uhalisia wa kifo katika
wimbo wake, kwa nini asingekuja na jeneza la imani yake? Angalia, jeneza lina
msalaba ambao unakubalika katika imani ya Kikristo, kwa nini asije na jeneza la
Kiislamu au sanduku ambalo halina msalaba?”
Akaongeza: Au inawezekana huyu jamaa anataka kubadili dini ili
aoane na Penny (Penniel Mungilwa) ambaye ni Mkristo kwa sababu huku ni kukana
imani yake kimyakimya.”
ALIWAHI KUTANGAZA KUJENGA
MSIKITI
Shabiki mwingine alikwenda mbali zaidi na kusema kama Diamond ni
muumini mzuri wa Kiislamu tena mwenye lengo la kujenga msikiti kama alivyowahi
kutangaza siku za nyuma, anatakiwa kutofungamana kabisa na ishara zinazoonesha
anaunga mkono imani nyingine.
“Anapaswa kuwa makini na mambo yake na awe na washauri wazuri,
vinginevyo atakuwa anafanya mambo yanayoibua maswali mengi kwa jamii
inayomwamini,” alisema shabiki huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la
Jennifer.
HUYU YUPO TOFAUTI
Shabiki aliyejitambulisha kwa jina la Hamadi Hajj (34) mkazi wa
Kijitonyama, Dar alisema:
“Hakuna uhusiano wowote kati ya hili jeneza na mambo ya
kubadilisha dini au kuiunga mkono. Kikubwa ni lengo alilotaka litimie.
“Ukiachana na hilo, mambo mengine yako wazi jamani. Upatikanaji wa
majeneza ya Kikristo ni rahisi zaidi tofauti na ya Kiislamu. Wabongo wanapenda
sana kukuza mambo,” alisema Hajj.
HUKU RISASI, KULE DIAMOND
Siku hiyohiyo, usiku huohuo, mapaparazi wetu walimbana Diamond
kuhusu kutinga Leaders na jeneza ambapo alijitetea hivi:
“Ni swaga tu zile.”
Alipobanwa zaidi na kuulizwa ni swaga gani zinazochanganywa na
vitu vinavyoashiria huzuni na imani ambayo si yake, alisema:
“Nilitaka kuwafurahisha mashabiki wangu na kuwapa uhalisia wa ule
wimbo wangu wa Nikifa Kesho, sikuwa na nia ya kukashifu imani ya mtu.”
FIESTA PART II
Baada ya shoo yake kushindikana na kuhamishiwa siku iliyofuata
(Jumapili), timu yetu ilitinga viwanjani hapo ili kujua kama Diamond angepanda
na jeneza hilo kama alivyotarajia lakini jeneza halikuwepo eneo lilipohifadhiwa
awali.
Diamond alipofuatwa na kuulizwa kama mpango wake bado uko
palepale, alijibu:
“Lile jeneza nilipanga kupanda nalo jukwaani wakati nikiwa naimba
wimbo wangu wa Nikifa Kesho lakini kwa bahati mbaya sikuweza kupanda kuimba
kutokana na matatizo ya kiufundi, leo (Jumapili) nisingeweza kupanda nalo kwa
kuwa muda tuliopewa ni mfupi sana,” alisema Diamond.
Alipobanwa kuhusu kutumia jeneza la Kikristo na kuhusishwa na
fununu za kubadili dini, alisema hana mpango huo kabisa.
“Naomba nieleweke, mimi sikuwa na nia tofauti zaidi ya kuwakilisha
kilichopo katika wimbo wangu. Lengo lilikuwa kuonesha uhalisia tu wa kibao
changu cha Nikifa Kesho, siyo zaidi ya hivyo,” alisema.
Inasemekana
kwamba Diamond aliamua kubadilisha uamuzi wake wa kupanda na jeneza jukwaani
siku hiyo baada ya kunyetishwa na watu wanaomtakia mema kuwa asingeonesha picha
nzuri kwa jamii, hasa kwa vile jeneza hilo lilikuwa na msalaba juu ya mfuniko.