Mwigamba alishushiwa kipigo hicho na baadhi ya viongozi
wenzake wa chama kwa madai ya usaliti na tayari amesimamishwa uongozi kwa muda
usiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas jana
alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na viongozi hao wa Chadema kufikishana
polisi.
Alikutwa na zahama hiyo mbele ya viongozi wakuu wa
Chadema Taifa, Mwenyekiti, Freeman Mbowe na mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei
katika Hoteli ya Coridal Spring.
Viongozi hao wamekuwa wakifanya ziara za aina hiyo nchi
nzima, kuimarisha chama na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa
mwakani na uchaguzi mkuu ujao wa Rais na wabunge mwaka 2015.
Habari kutoka ndani ya mkutano huo zinaeleza kuwa hatua hiyo
ilifuatia tuhuma kwamba Mwigamba alituma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa
Jamii Forums, unaodaiwa kukichafua chama hicho.
Tukio hilo la aina yake lilitokea wakati viongozi wote
wa juu wa chama hicho, wakiongozwa na Mbowe walipokuwa wakijadili mustakabali
wa chama hicho, mkutano ambao ulihudhuriwa na wabunge karibu wote wa Chadema wa
kanda hiyo.
Hata hivyo, wakati mijadala ikiendelea baadhi ya
viongozi wa chama hicho, akiwamo Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema
walimtuhumu Mwigamba kutuma ujumbe kwenye mtandao huo, uliokuwa ukizungumzia
ufisadi ndani ya chama hicho, wakidai alitaka Mwenyekiti Mbowe kukubali
kuchunguzwa.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana, Mwigamba alisema
kuwa baada ya Lema kutoa tuhuma hizo aliungwa mkono na viongozi wengine na
vijana waliokuwa wameimarisha ulinzi, kumvamia na kuanza kumpiga pamoja na
kumnyang’anya kwa nguvu kompyuta mpakato (Laptop), aliyokuwa nayo, kisha
kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi, mjini Arusha.
“Wamenipiga sana na kuniweka ndani, ila nashukuru Mkuu wa
Upelelezi wa Wilaya ya Arusha (OCCID), alikuja na kunitoa saa 5:00
asubuhi,” alisema Mwigamba.
Alisema kuwa leo katika mkutano wake na waandishi wa habari
ataeleza yote yaliyotokea na hatua atakazochukua, kwa kuwa yeye ni
kiongozi wa juu wa chama.
Hata hivyo, alieleza kwamba bado
anashauriana na wanasheria wake kuona kama anaweza kuwachukulia hatua
waliompinga.
Kauli ya polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus
Sabas alisema polisi wameona hakuna kosa la kisheria lililotokea hasa kutokana
na malalamiko yaliyofikishwa kwao dhidi ya Mwigamba ya kukichafua chama kwenye
mitandao.
“Hili suala la mitandao ni kubwa na lina
taratibu zake sasa kusema tu umechafuliwa na iwe kesi nadhani uchunguzi
unahitajika kwao, sisi tumeona haya ni mambo yao wanaweza kuyamaliza wao ndiyo
sababu tulimwachia, Mwigamba,” alisema Sabas.
Kosa analodaiwa kufanya Mwigamba
Akizungumzia sakata hilo jana, Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kwamba Mwigamba alibainika kutuma
ujumbe kwenye mtandao wa Jamii Forums uliokichafua chama hicho, akieleza
haikuwa mara yake ya kwanza kwa kiongozi huyo kufanya hivyo na kwamba walikuwa
wakimfuatilia kwa muda mrefu.
“Kilichotokea ni hicho, vijana wa Red
Brigade ndio waliomtoa ukumbini, baada ya kumbaini kukichafua chama, kwani
laptop yake baada ya kuchunguzwa na wataalamu wetu walijiridhisha ni yeye ndiye
aliyetuma ujumbe huo,” alisema Lema.
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani
Golugwa alitaja tuhuma zinazomkabili Mwigamba kuwa ni pamoja na kusema uongo,
kupotosha taarifa za chama na kuchonganisha viongozi kupitia mtandao wa kijamii
ya Jamii Forums.
Katika andiko lake kwenye mtandao, Mwigamba
anadaiwa kuwatuhumu viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Taifa,
Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa kuwa wamechakachua katiba ya
chama hicho kuhusu ukomo wa nafasi za uongozi ili kujinufaisha binafsi.
Golugwa alisema kuwa baada ya kubanwa kwenye
kikao, Mwigamba alikiri kuandika na kurusha taarifa hizo kwenye mitandao,
lakini alipotakiwa kukabidhi kompyuta yake ili ichunguzwe na wataalamu wa
mawasiliano wa chama hicho aligoma, hali iliyozua tafrani kati yake na walinzi
wa chama hicho (Red Brigade), waliolazimika kutumia nguvu kumdhibiti.
Purukushani zilivyotokea
Habari zaidi zinaeleza kuwa katika harakati za
kutaka kumnyang’anya Mwigamba kompyuta yake, mwenyekiti huyo wa Chadema mkoani
Arusha alianza kushambuliwa na baadhi ya viongozi wa Chadema, kabla ya
kufanikiwa kumdhibiti.
Zinaeleza kuwa katika
tukio hilo kulitokea pia kurushiana maneno na matusi ya nguoni kati yake na
viongozi wengine wa chama hicho akiwamo Lema.
Baadaye Lema aliliambia gazeti hili kwamba
katika purukushani hizo Mwigamba alimrushia ngumi ambayo hata hivyo aliikwepa.
Alisema kuwa wanakusudia kumfungulia
kesi Mwigamba ya kukichafua chama chao katika mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, alisema kikao chao
kiliendelea jana bila ya vurugu zozote na kuweka mikakati ya kushinda majimbo
yote ya Kanda ya Kaskazini mwaka 2015 na kuchukua nchi katika uchaguzi huo
ujao.
Adhabu kwa Mwigamba
Katika hatua nyingine Chadema, kimemsimamisha uongozi
Mwigamba kwa tuhuma za kukisaliti, kukihujumu chama hicho na viongozi wake.
Akitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa
habari jijini Arusha jana, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel
Natse alibainisha kuwa uamuzi wa kumsimamisha Mwigamba katika nyadhifa zote za
uongozi ndani ya chama ulifikiwa na kikao cha Baraza la Uongozi wa Kanda ya
Kaskazini kilichokutana juzi.
Alisema kuwa Mwigamba amesimamishwa kwa muda
usiojulikana kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na kuonya kuwa iwapo tuhuma
zitathibitishwa, hatua nyingine za kinidhamu zitafuata kulingana na kanuni na
katiba ya Chadema.
“Kwa sasa Mwigamba anatuhumiwa kuvunja sura ya
kumi, kifungu cha 10.1 kifungu kidogo cha 8, 9 na 10 ya katiba ya Chadema
inayozungumzia maadili ya uongozi,” alisema Natse.
Akifafanua zaidi alisema
kuwa sura na vifungu hivyo vinakataza kiongozi wa chama hicho kutoa tuhuma
dhidi ya viongozi wenzake bila kufuata vikao halali vya kikanuni na kikatiba.
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako