Sunday 13 October 2013

MECHI YA YANGA VS KAGERA YAINGIZA ZAIDI MILIONI 20 KAITABA



MCHEZO wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo kati ya wenyeji, Kagera Sugar na Yanga SC umeingiza kiasi cha Sh. Milioni 20. 5, wakati kila klabu imepata mgawo wa Sh. Milioni 4.9.
Taarifa kutoka Chama cha Soka Kagera (KRFA) usiku huu, imesema kwamba jumla ya Sh 20, 525,000 zimepatikana na kila timu imepata Sh. 4,907,000.
Katika mchezo huo, ambao Yanga SC imeibuka na ushindi wa 2-1, Sh. 3,139,320 ni makato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), gharama za Uwanja Sh. 2,495,000 na gharama za mechi Sh. 1,497,000.

Makato mengine ni mgawo wa Kamati ya Ligi Sh. 1,497,000, KRFA 582, 100 na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepata Sh. 748,543.
Mabingwa watetezi Yanga SC wamepata ushindi wa kwanza ugenini msimu huu baada ya kuilaza Kagera Sugar mabao 2-1, hivyo kupaa hadi nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 15, nyuma ya Simba SC yenye pointi 18.
Yanga SC walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya pili mfungaji Mrisho Ngassa aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kurushwa wa beki wa kulia Mbuyu Twite, kabla ya Kagera kusawazisha dakika ya 47 kupitia kwa Godfrey Wambura na Hamisi Kiiza kufunga la ushindi dakika ya 59.      
Katika mechi nyingine za leo, bao pekee la kiungo Jonas Mkude dakika ya 62 lilitosha kuipa Simba SC ushindi wa 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Ashanti United iliilaza 2-1 Coastal Union ya Tanga.
Mabao ya Ashanti yalifungwa na Tumba Sued dakika ya 23 kwa penalti na 88 wakati la Coastal lilifungwa na Jerry Santo kwa penalti dakika ya nne.

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako