Thursday 17 October 2013

VIJANA WAKITANZANIA WALIOKO KWENYE SELO ZA CHINA NA HONGKONG



VIJANA wa Kitanzania takriban 175 wapo katika magereza ya nchini China kutokana na makosa ya uhalifu yakiwamo ya kusafirisha dawa za kulevya.
  
Taarifa hiyo ilitolewa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali mstaafu, Abdulrahman Shimbo, baada ya kiongozi huyo kuwasili nchini humo.
  
Shimbo alisema kuwa kati ya hao, watatu uraia wao ni wa kutiliwa shaka. 48 wako China Bara, Hong Kong wapo 117 na Macao wapo 10.
  
Alisema kuwa wanawake ni 34, ambapo 28 wako Hong Kong na sita wako China Bara.

Akizungumza na maofisa wa ubalozi pamoja na wajumbe wa msafara wake, Pinda alisema tatizo la dawa za kulevya linaharibu sifa ya Tanzania pamoja na mahusiano baina yake na nchi marafiki.
  
“Tunahitaji kufanya kazi ya ziada ili kupambana na wasafirishaji wa dawa za kulevya. Watu 175 ni wengi kwa nchi moja lakini cha kusikitisha zaidi idadi kubwa ni ya wanawake waliokamatwa,” alisema.
  
Kuhusu misaada ya China kwa Tanzania, alisema kuna miradi ya kufa na kupona ambayo itabidi iwekewe uzito katika ziara yake hii na kuiainisha kuwa ni ujenzi wa Reli ya Kati, usambazaji wa umeme na ukuzaji wa utalii baina ya nchi hizo hasa fursa ya kuanzisha usafiri wa ndege wa moja kwa moja baina ya China na Tanzania.
  
Leo Pinda atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Li Keqiang, Rais wa Benki ya Exim ya China, Rais wa Benki ya Maendeleo ya China na uongozi wa China Railway Jianchang Engineering. Pia atahudhuria dhifa ya taifa itakayoandaliwa kwa heshima yake kesho jioni.
  
Mapema, Balozi Shimbao alimweleza waziri mkuu kuwa sehemu kubwa ya utekelezaji wa miradi kati ya Tanzania na China iko chini ya mwamvuli wa FOCAC (Forum on Africa China Co-operation) ambayo inagawanyika katika maeneo sita.
  
Pinda aliwasili Beijing, China jana jioni na kuanza vikao ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku tisa, kwa mwaliko wa serikali ya nchi hiyo.


No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako