Azam Media Limited imefanikiwa kukamilisha
utaratibu wa ushirikiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
utakaowawezesha mashabiki wa kandanda kote nchini kunufaika kwa kuona michezo
ya Ligi Kuu ya Vodacom kila mwishoni mwa juma hadi kukamilika kwa nusu ya msimu
wa 2013/14 kupitia TBC1 kwa hisani ya AzamTV.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na
Bodi ya Ligi (Kamati ya Ligi) wameeleza kuunga mkono utaratibu huu makini.
“Baada ya kupata haki za matangazo ya luninga
ya Ligi Kuu ya Vodacom, moja ya shabaha zetu kuu imekuwa ni kuhakikisha kuwa
tunafanikiwa kurusha matangazo yanayokidhi viwango vya kimataifa kwa ubora. Ili
kufanikisha shabaha hiyo tumewekeza vilivyo katika teknolojia ya kisasa ya
vifaa vya matangazo ya nje (Outside Broadcasting) na katika mafunzo kwa
watumiaji wa vifaa hivyo.
Ninayo furaha kusema kuwa matayarisho
yamekwenda vema kiasi kwamba tumejikuta tuko tayari kurusha matangazo ya
kiwango cha juu kabla hata ya kuzinduliwa kwa huduma kamili za AzamTV”, alisema
Rhys Torrington, Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited.
“Kwa kuwa mashabiki wengi kote nchini
wanangojea kwa hamu kubwa kuziona timu wazipendazo, imeonekana ni vema kuanza
kuonesha michezo hii ya Ligi sasa. Kwa kuzingatia hali hiyo, nilifanya
mazungumzo na rafiki zetu pale TBC na kuwaomba iwapo wana uwezo na
kuridhia kurusha matangazo yetu ya moja kwa moja bila ya malipo
yoyote kuanzia mwisho wa juma hili hadi kukamilika kwa nusu msimu.
Tulifanikiwa kufikia makubaliano kwa
haraka na sasa tunafanyia kazi masuala ya kiufundi yatakayowezesha kuwa tayari
kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi utakaofanyika Uwanja wa Taifa”, Aliongeza Bw.
Torrington.
Mara tu
huduma kamili za AzamTV zitakapozinduliwa majuma machache yajayo, matangazo ya
michezo ya Ligi Kuu kwa wigo mpana yatakuwepo pia kwenye chaneli yake hadi
mapumziko ya nusu msimu. Baada ya hapo matangazo ya Ligi Kuu ya Vodacom
yatapatikana kwa wale tu watakaokuwa na visimbuzi (decorders) vya AzamTV.
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako