Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametembelea
eneo la Dumila ambako mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zimesababisha mafuriko
ambayo yameharibu sehemu ya barabara kwenye daraja la Mto Mkundi mkoani
Morogoro.
Akiwa katika eneo hilo Waziri Magufuli baada ya kujionea
hali halisi amemwagiza Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tanroads Mhandisi Crispianus Ako
pamoja na Watendaji wengine waandamizi kutoka Tanroads na Wizara ya Ujenzi
kuwepo hapo muda wote wakati kazi za kurejesha mawasiliano zikiendelea ili kuhakikisha
kuwa matengenezo hayo yanakamilika mapema tayari kwa magari kuanza kupita.
Katika hatua nyingine Mhe. Magufuli ametahadharisha kuwa
magari yanayoruhusiwa kuzungukia barabara mbadala inayoanzia Dumila kupita
Kilosa hadi Morogoro ni mabasi ya abiria na magari mengine yasiyozidi uzito wa
tani 10. “Barabara hii mbadala ya kupitia Kilosa, Melela hadi Morogoro ni ya
mkoa na iko katika kiwango cha changarawe ikiwa na madaraja yenye uwezo wa
kubeba chini ya tani 10 tu, hivyo magari mengine yote yenye uzito zaidi ya hapo
yatabidi kusubiri wakati tukiendelea na jitihada za kuifungua barabara hii
mapema iwezekanavyo” amefafanua Mhe. Magufuli.
Daraja la Mkundi liko kiasi cha kilometa 65 kutokea Morogoro
mjini kuelekea Dodoma na mikoa mingine ya kati hadi magharibi mwa nchi yetu
ikiungana na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya watu wa
Kongo.
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako