Saturday 14 December 2013

UGOMVI WA KIMAPENZI WAPELEKEA MUME KUUA MTOTO WA KAMBO IRINGA

KATIKA  hali  isiyo ya kawaida mwanaume  mmoja mkazi  wa mtaa wa Pangani kata ya Makorongoni  katika Manispaa ya Iringa Hamis Said maarufu kwa jina la Mwarabu amemuua kinyama mtoto Raymond Ben Mangungu (2) kutoka na ugomvi wa kimapenzi  kati  yake na mama wa mtoto  huyo ambae kwake ni mpenzi wake.
Imedaiwa  kuwa  mtuhumiwa  huyo  wa mauaji ya mtoto huyo  alikuwa amelewa  pombe kupita kiasi na si mara ya kwanza  kulewa kiasi hicho na  kutishia kufanya mauaji dhidi ya mtoto  huyo wa kambo kwa kile alichokuwa akidai kuwa ni fedhea kwake  kuishi na mwanamke ambaye ana watoto wawili ambao si damu yake.
Wakizungumzia juu ya tukio hilo mashuhuda wa tukio hilo kwa sharti la  kutotaja majina yao  walisema  kuwa imekuwa ni kawaida  kwa Mwarabu kumpiga mwanamke huyo na familia yake kwa madai kuwa hataki kuwaona  watoto hao wakiendelea kuishi katika nyumba hiyo ambayo ameipanga  yeye.
"Huyu  bwana Mwarabu alikuwa akifanya kazi ya kuuza korosho  mitaani na akirudi usiku amekuwa mkali kwa mwanamke  huyo ambae  alikuwa akidai kuwa bado amekuwa na mahusiano na baba  wa  watoto  hao  wawili .....hata  hivyo sisi kama majirani  tumekuwa  tukishindwa  kuwaamua kutokana na mwanaume  kuwa na tabia ya kulewa pombe kupita kiasi na hata tukio hili tulijua ni kawaida yao"
Mtoto Tinito Mangungu (6) ambae ni kaka na marehemu alisema  kuwa baba yao huyo mdogo alifika usiku na kuwataka wote  kuamka kitandani na kuwa hakuna mtu atakayelala katika chumba  hicho kama si damu yake.
"Baba mdogo (Mwarabu) alirudi usiku akiwa amelewa na kusema hakuna mtu  kulala kitandani na kuanza kumpiga mama kwa meza na viti  huku sisi tukilia kumtaka asimpige  mama yetu....baada ya hapo alimchukua mdogo  wangu na kuanza kumkaba shingo na kumwacha  kitandani akiwa amelala bila kuamka hadi sasa mama anasema amekufa"
Akielezea  juu ya mkasa huo uliosababisha mauaji ya mtoto Raymond mama mzazi wa mtoto huyo Bi Kudra Kahemela (23) alisema  kuwa kwa upande wake baada ya kutishiwa kuuawa kwa  kipigo alifanikiwa kukimbia katika chumba hicho na kwenda  kujificha nje na baada ya muda mwanaume huyo alianza kutapika na pale alipoingia kutaka kumsaidia ndipo alipopigwa na kuamua kukimbia kwenda kulala nje ya nyumba  hiyo kwa kujiegesha katika nguzo ya umeme iliyopo nyumba ya pili karibu na nyumba ya  shekhe wa  mkoa Juma Alli Tagalile
Alisema  kuwa asubuhi aliingia katika  chumba  hicho baada ya mwanaume  huyo  kutoka kwenda katika kilabu cha pombe za kienyeji cha Tulivu kuendelea kunywa pombe na kumkuta mtoto  huyo akiwa amelala bila kutikisika
"Mimi  nilijua kama mtoto amelala tu ama amezimia ila baada ya  kuwaita watu  wazima akiwemo mama yangu mzazi ndipo  nilipobaini  kuwa mtoto  wangu Ray amefariki  dunia na ndipo  nilipomfuata na kumweleza juu ya tukio hilo ila bado aliendelea  kunywa pombe na kudai kuwa mtoto huyo amezimia kwa kelele za usiku"
Alisema baada ya hapo mwanaume huyo alikimbia hadi Ilala kwa wakwe zake na kuomba msamaha na kusuruhishwa ugomvi wao  ila wakati huo mtego wa kukamatwa ukiwekwa ndipo alipokimbia kusikojulikana.
Mwandishi wa habari hizi  alishuhudia mtoto huyo akiwa amekufa  katika  kitanda cha wazazi wake huku chini ya chumba hicho  thamani mbali mbali pamoja na vyombo vikiwa vimevunjika kutokana na ugomvi huo
Mwenyekiti  wa Serikali ya  mtaa huo wa Pangani kata ya Makorongini Bw. Salum Kibaya amethibitisha juu ya kifo cha mtoto huyo na kuwa baada ya tukio hilo ambalo lilitokea usiku wa kuamkia leo Jumamosi Desemba 14 mwaka huu alilazimika kwenda kituo cha polisi cha stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani na kuwajulisha juu ya tukio hilo na kufika eneo la tukio.
Bw  Kibaya  alithibitisha pia kuwa ugomvi kati ya wapenzi hao si wa kwanza kutokea japo kwa maelezo ya mwanamke huyo alikuwa mbioni kuolewa na mwanaume huyo na hivyo kuwa na wanaume wawili akiwemo mzazi mwenzake ambae kwa sasa anaishi eneo la Don Bosco mjini hapa.
Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa huku jeshi la polisi likiwahoji mama wa mtoto  huyo, kaka wa mtuhumiwa wa mauaji  hayo ambaye ni mkazi wa Mlandizi Kibaha Jijini Dar es Salaam  na mama mzazi  wa mtoto aliyepoteza maisha.

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako