Sanamu
kubwa zaidi duniani ya Nelson Mandela imezinduliwa katika mji mkuu wa Afrika
kusini Pretoria siku moja baada ya rais huyo wa zamani kuzikwa. Sanamu hiyo
iliyotengenezwa kwa shaba ina urefu wa mita tisa na ina uzani wa tani nne
unusu. Ilizinduliwa katika bustani la majengo ya bunge na inaonyesha Nelson
Mandela akihimiza umoja na maridhiano.
Sanamu hiyo yenye mikono ya Mandela
ikiwa wazi ilinuia kuonyesha Mandela alivyoliunganisha taifa zima kwa mapenzi
yake. Marehemu Mandela alipewa mazishi ya kitaifa nyumbani alikozaliwa katika
kijiji cha Qunu Jumapili Familia ya Madiba, viongozi wa ANC, viongozi wa Afrika
na maafisa wengine wakuu walihudhuria mazishi hayo katika kijiji cha Qunu
mkoani Cape Mashariki. Kifo cha Mandela kilifuatwa na maombolezi ya siku kumi
na sherehe za kukumbuka maisha ya Mandela aliyefariki akiwa na umri wa miaka
95.
Bendera ya nchi hiyo ilirejeshwa kupepea katika urefu wake wa kawaida.
Mandela anakumbukwa kwa juhudi zake za kupatanisha wananchi na kupigia debe
msamaha miongoni mwa watu na ndio maana leo ikawa siku iliyotengwa kwa ajili ya
uzinduzi wa sanamu hiyo. Wakati wa utawala wa wazungu, terehe 16 Desemba
ilijulikana kama siku ya kuwakumbuka mashujaa wa Afrikaners walioshinda vita
dhidi ya jeshi la Zulu mwaka 1883. Zaidi ya karne moja baadaye mwaka 1961,
Mandela alizindua jeshi lake la Umkhonto we Sizwe kupigana dhidi ya utawala wa
wazungu.
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako