Saturday 21 December 2013

KIKWETE ATENGUA NYADHIFA ZA MAWAZIRI WANNE


Kufuatia majadiliano yanayoendelea Bungeni kuhusu ripoti iliyotolewa na kamati ya ardhi maliasili na utalii, Rais Jakaya Kikwete ametengua majukumu ya mawaziri wanne kufuatia shutuma nzito dhidi yao katika sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili 
Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Maliasili na Utalii
Mawaziri hao ni wa wizara za Maliasili na Utalii,Mambo ya Ndani, Ulinzi na jeshi la kujenga Taifa, pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Emmanuel Nchimbi, Waziri wa mambo ya Ndani
Kufuatia maamuzi hayo mawaziri wa Wizara hizo ambao ni Balozi Khamis Kagasheki, Shamsi Vuai Nahodha, Emmanuel Nchimbi na Mathayo David Mathayo wameondolewa rasmi nyadhifa zao za uwaziri katika wizara hizo hadi uamuzi mwingine utakapotangazwa na Rais.
Mathayo David Mathayo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Akizungumza Bungeni Dodoma usiku huu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikiri kulikuwa na matatizo makubwa katika usimamizi wa zoezi hilo.
Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
“Tulifanya operesheni kwa nia nzuri,” alisema Waziri Mkuu Pinda. “Tatizo ni namna operesheni hiyo ilivyotekelezwa.”
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitangaza Maamuzi ya Rais Jakaya Kikwete
Katika mdahalo uliogusa nyoyo za wabunge na wachambuzi mbalimbali wa siasa leo, wabunge waliueleza umma jinsi ambavyo Operesheni hiyo ilitumika kutesa, kunyanyasa na kuua raia wasio na hatia na kuwadhulumu mali zao. 

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako