Wednesday, 4 September 2013

MICROSOFT YANUNUA HISA KAMPUNI YA NOKIA

Ikiwa ni miaka miwili tu tangu kuwekeza kwenye mfumo wa simu wa kampuni kubwa ya tarakilishi, Microsoft (Windows Phone), kampuni iliyovuma sana kwenye soko la simu za mkononi, Nokia, imeangukia moja kwa moja mikononi mwa Microsoft kwa kukubali kuuza simu zake kwa jumla ya euro bilioni 5.44 (sawa $7.2 bilioni).
Nokia, kampuni tanzu ya Ufini (Finland) imekubali Microsoft kampuni tanzu ya Marekani, kuipa umiliki wa simu za kisasa zinazotumia mfumo wa Lumia ambao unatumika kwenye mfumo wa simu za Windows za Microsoft. Microsoft italipa $5 bilioni kununua vifaa na huduma za Nokia na itaongeza $2.2 kusajili 'patent' za Nokia.
Biashara nzima inatarajiwa kufungwa rasmi mwanzoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2014 ikiwa  wadau na wasimamizi wataafiki. Kampuni hizo kubwa zimekuwa zikifanya kazi kwa ushirika wa karibu tangu mwezi Februari mwaka 2011 kwa malengo ya kutengeneza simu za kisasa ambazo zingepambana na simu za kisasa za kampuni za Apple (Marekani) na Samsung (Korea Kusini). 

Nokia ni kampuni yenye umaarufu zaidi katika nchi za mabara ya Ulaya, Afrika na Asia lakini bado imeshindwa kujipenyeza hivyo
kwenye soko la Marekani ingawaje imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupiku soko linalosua sua la BlackBerry na kuchukua nafasi ya tatu kwenye makampuni makubwa ya simu za kisasa.

Wadadisi wa mambo wanasema hatua hii ya Microsoft kuinunua Nokia inaashiria kuwa imenuia kuwa kampuni ya kutengeneza vifaa hivyo zaidi (more of a devices company) ya kutengeneza mifumo ya kuendesha vifaa vyenyewe (less of a software company).
Hii ni mara ya pili kampuni ya Microsoft inatoa kiasi kikubwa kabisa cha fedha na kununua sehemu ya kampuni nyingine kubwa, baada ya kufanya hivyo mwezi Mei 2011, ilipoinunua kampuni ya simu za kwenye iternet, Skype kwa kiasi cha $9.3 bilioni. Yaelekea ndoto zake ni kubwa kwani iliota kuhakikisha kuwa

inaweka kompyuta katika kila meza ya ofisi na sasa inanuia kuweka simu katika kila mfuko wa nguo.
Ikiwa itafanikiwa ama itafeli, walengwa tunasubiri kujionea. 

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako