Tuesday, 24 September 2013

BASI LA AL SAYEED LAUA WATU 6



Watu sita wamefariki dunia na wengine 34 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Chinangali wilayani Chamwino mkoani Dodoma baada ya basi la kampuni ya Al Sayeed lililokuwa likitokea jijini Dar-Es-Salaam kwenda Dodoma kugongana uso kwa uso na lori la mizigo lililobeba shehena ya mahindi likitokea Dodoma kwenda Dar es salaam.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Mrakibu Mwandamizi Damas Nyanda amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa basi hilo lenye namba za usajili T 433 BLR aina ya Youtong ambaye alishindwa kulimudu na kuacha njia na kulivaa lori aina ya Layland Daf lenye namba za usajili T 102 CGR likiwa na tela lenye namba za T 928 na kusababisha watu watano kufariki papo hapo.
 
ITV ilifika katika eneo la tukio na kuzungumza na baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo na wamelalamikia uhaba wa vyombo vya uokoaji ambapo wamesema kama vyombo vya uokoaji vingefika kwa wakati huenda watu wote wanne waliofariki kwenye lori wangeokolewa.
Nao baadhi ya majeruhi waliolazwa katika hosipitali ya rufaa ya Dodoma wamesema kabla ya kutokea kwa ajali hiyo dereva wa basi hilo alikuwa katika mwendo kasi na baada ya kuliona lori hilo alifunga breki za ghafla na kusababisha basi hilo kulivaa lori hilo huku mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dk Mzee Nasoro akasema walipokea majeruhi 20 na mmoja kati yao amefariki dunia

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako