Mshambuliaji wa nyota wa zamani wa timu ya soka ya Simba na Taifa,
Joseph Kaniki ‘Golota’ na bondia Mkwanda Matumla wanashikiliwa huku Addis
Ababa, Ethiopia wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya.
Kukamatwa kwao kumezidi kuongeza idadi ya Watanzania maarufu waliotiwa
mbaroni nje ya nchi katika siku za karibuni wakituhimiwa kwa makosa hayo.
Tukio hilo limetokea miezi miwili baada ya Watanzania wawili, wasanii
Agnes Gerald Masogange na Melisa Edward kukamatwa kwenye Uwanja wa Oliver
Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa
kilo 150 na thamani ya Sh 6 bilioni.
Aidha, hilo limetokea baada ya meli ya mizigo ya Gold Star
iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa Forodha na askari wa doria wa Italia
katika Pwani ya Sicily, Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa za
kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni za Uingereza 50milioni (Sh125
bilioni).
Kaniki na Matumla walikamatwa Agosti 31, mwaka huu kwenye Uwanja wa
Ndege wa Bole, Addis Ababa wakati wakijiandaa kupanda ndege ya Shirika la Ndege
la Ethiopia tayari kwa safari ya kuelekea Paris, Ufaransa.
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Samuel Shelukindo
alithibitisha jana kwamba wanamichezo hao wanashikiliwa nchini humo na Polisi
wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai.
Wanamichezo hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakamu Kuu ya Ethiopia
iliyoko kwenye eneo la Arada, Addis Ababa kujibu tuhuma za kubeba kilo saba za
dawa hizo haramu. Mkwanda anadaiwa kubeba kilo nne wakati Kaniki akidaiwa
kubeba kilo tatu. Kama watapatikana na hatia, wanaweza kufungwa kifungo cha
miaka tisa hadi 15.
Alisema uwezekano wa kesi ya Kaniki na Matumla kurudishwa Tanzania
haupo kwa kuwa nchi hizi mbili hazina utaratibu wa kubadilishana wafungwa.
“Wameshikiliwa hapa Ethiopia kwa zaidi ya siku 10 sasa, sisi tulipigiwa
simu na polisi wa hapa Alhamisi iliyopita kujulishwa kwamba kuna Watanzania
wawili wameshikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, tulipokwenda
tukamkuta ni Kaniki na Matumla,” alisema Shelukindo.
“Wao wenyewe wanaeleza kwamba walipitia Mombasa na huo mzigo walipewa
na mtu mmoja. Lakini Kaniki yeye anajitetea kwamba huyo aliyewapa huo mzigo
pale Mombasa anajuana vizuri na Mkwanda. “Kwa hiyo alichofanya yeye ni kuubeba
tu. Walikuwa wapitie hapa Addis wakashuke Paris, Ufaransa ndipo warudi Sweden
kwa njia zao wanazojua wenyewe. Walipofika hapa Mkwanda alifanikiwa kupenya
akapanda ndege lakini Kaniki akanaswa na mbwa ndipo akajitetea kwa polisi
kwamba lile begi lilikuwa lake lakini mizigo mingine ilikuwa ya Mkwanda.
“Ndipo hapo sasa Mkwanda akashushwa kwenye ndege wakashikiliwa na
Jumatatu ya wiki iliyopita wakapandishwa kwenye Mahakama ya hapa kutajiwa kesi
yao lakini hawakupewa nafasi ya kujitetea. Kesi itatajwa tena Jumanne (leo) na
Jumatano (kesho) na uchunguzi wa polisi bado unaendelea.”
Wanamichezo hao walidai kwamba walikabidhiwa mizigo hiyo kwenye Uwanja
wa Ndege wa Mombasa walipokuwa wakikabidhiwa pasi za kupandia ndege baada ya
kupita sehemu zote za ukaguzi.
“Kilichotokea ni jambo la aibu kwa nchi na hata wachezaji wenyewe
wanajuta. Kwa mfano, Kaniki anasema alikuwa aende England kucheza mpira Desemba
lakini sisi tukamwambia hatuwezi kumsaidia inabidi akabiliane na kesi iliyoko
mbele yake. Mkwanda yeye ametuambia kwamba anaishi Sweden hatuna maelezo yake
zaidi,” alisema Shelukindo na kuongeza kuwa wamewapelekea wanamichezo hao
msaada wa mablanketi kwa vile bado wako mahabusu na Ethiopia kwa sasa kuna
baridi kali.
Shelukindo alisema wachezaji hao wapo mahabusu kwenye Kituo cha Polisi
cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (Federal Police Crime Investigation) na hawana
chochote zaidi ya nguo walizokuwa wamevaa.
Watanzania wengine kuachiwa leo
Shelukindo alisema kuna Watanzania wanne wanaotazamiwa kuachia leo
baada ya kumaliza vifungo vyao baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa
za kulevya.
“Kuna Watanzania wengine
walinaswa hapa miaka ya nyuma wao walikuwa wamemeza wakapasuliwa dawa
zikatolewa na baadhi yao walifariki. Hata hivyo, wanne ambao wamemaliza vifungo
vyao vya miaka minne wanaweza kurudishwa Tanzania,” alisema Shelukindo
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako