Mkuu wa Wilaya ya
Mbulu, mkoani Manyara, Anatory Choya, amesema kuwa aliwapigia magoti wananchi
wa Kijiji cha Hydom, ili kuonyesha unyenyekevu kwa wananchi hao aliodai
walionekana kujazwa maneno ya uchochezi na wanasiasa ili wavuruge amani .
Alisema kutokana
fujo zilizofanywa na baadhi ya wananchi hao katika mkutano wa hadhara
uliofanyika majuzi, kwa nafasi yake angeweza kuagiza hata Jeshi la Polisi
kuwadhibiti watu, lakini misingi ya dini yake haimruhusu kumdhuru mtu zaidi ya
kumwonyesha unyenyekevu.
Alisema hali hiyo
ndiyo iliyomfanya kuamua kupiga magoti na kumshtakia Mungu.
“Mimi ni mkristo,
unyenyekevu ndiyo nguzo pekee ya kuonyesha upendo na kudumisha amani. Ningeweza
kuagiza polisi wawadhibiti, lakini sioni sababu kwa kuwa hiyo siyo misingi ya
utawala. Ndiyo maana nikaona bora nitumie njia nyingine ya kumshirikisha Mungu
mbele yao,”alisema Choya na kuongeza:
“Wanasiasa
wamekuwa wakipandikiza chuki kwa wananchi kwa makusudi kwa lengo la kuvuruga
amani lakini kwa kumweka Mungu mbele nina imani tutafanikiwa ili siku moja
tusije tukaingia kwenye mkumbo wa Syria na Misri”
Choya alitoa kauli
hiyo jana alipokuwa akizungumza na Mwananchi Jumapili, siku chache baada ya
kitendo chake cha kupiga magoti mbele ya wananchi kwenye mkutano wake wa
hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Haydom.
Mkuu huyo wa
wilaya alidaiwa pia kuwalaani baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Haydom kwa kile
kinachodaiwa kuwa ni kumdharau na kutofuata maagizo yake, wakati yeye
amewasaidia katika kutatua migogoro mbalimbali waliyokuwa nayo.
Tukio hilo la
kusikitisha lilijitokeza baada ya wananchi wa kijiji hicho kupinga agizo la
Choya, lililowataka kufanya uchaguzi wa kaimu mwenyekiti wa kijiji hicho, kabla
ya kufanya uchaguzi mdogo, ambapo walipinga kwa kudai kuwa hakuna sheria hiyo.
Mmoja wa wananchi
hao alilumbana na mkuu huyo wa wilaya ambapo Choya alijibu; “Nami nitarudi
kwetu.” Naye Tikin akasema tena: “Unasema utarudi kwenu Biharamulo wakati
hawakutaki kwani ulifukuzwa ubunge?”
Maneno hayo
yalionyesha kumkwaza Choya ambapo alipiga magoti huku machozi yakimlenga na
kumwomba Mungu afanye jambo kwa watu wa Haydom kwani wanamdharau kabla ya
kujitokeza wazee watatu wa Haydom na kumwomba msamaha mkuu huyo wa wilaya.
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako