MTALII mmoja raia wa Marekani, Thomas Macfee (58), ameuawa na kundi la
tembo wakati akiwa kwenye kambi ya Kakoi Tarangire eneo linalodaiwa kuwa ni
mapito ya asili ya wanyama hao.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Musa Marambo, alisema kuwa
tukio hilo lilitokea Agosti 30 mwaka huu, saa 2:30 asubuhi baada ya mtalii huyo
akiwa na wenzake watano ambao majina yao hayakupatikana kujaribu kupiga picha
za kundi kubwa la tembo lililokuwa likipita karibu na eneo walilokuwa.
Alisema kuwa wakiwa kwenye harakati za kupiga picha, ghafla tembo hao
walibadili uelekeo na kuanza kuwafuata ndipo wakaanza kukimbia ambapo kwa
bahati mbaya Macfee alinasa kwenye dimbwi la matope.
“Baada ya kunasa kwenye matope alishindwa kutoka ndipo tembo wale
wakaanza kumpitia juu na baada ya hapo wenzake walienda kumchukua na
kumuwahisha kwenye zahanati ya hifadhi ya taifa ya Tarangire ndipo akafariki,”
alisema Manyara.
Alisema kuwa baada ya kufariki alipelekwa kuhifadhiwa kwenye hospitali
ya Selian jijini Arusha ambapo ubalozi wa Marekani ulimchukua kwa ajili ya
taratibu za mazishi.
Meneja uhusiano wa Tanapa, Paschal Shelutete, alitoa taarifa kwa
vyombo mbalimbali vya habari akifafanua kuwa eneo alilokuwa mgeni huyo ni nje
ya hifadhi yao.
“Tukio la mgeni husika lilitokea nje ya hifadhi ya Tarangire katika
kijiji cha Kakoi kambi ya Tarangire River Camp, wakiwa wanafanya utalii wa
kutembea kwa miguu.”
“Baada ya kuvamiwa na kuumizwa, mgeni huyu alifikishwa katika zahanati
ya Tarangire na watumishi wa kambi aliyofikia ambayo iko nje ya hifadhi kwa
ajili ya matibabu ya huduma ya kwanza ambapo alifariki,” alisema.
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako