Ilikuwa siku ya Alhamisi tarehe kama ya leo (Septemba
8,) miaka TISA iliyopita wakati Globu ya Jamii ilipozaliwa rasmi katika ukumbi
wa mikutano wa Finlandia jijini Helsinki Finland, kama utani tu. Kwa msemo
mwingine, ni miaka TISA kamili leo toka Globu ya Jamii ianze Libeneke la
kuhabarisha wadau kwa mapicha na habari kemkem bila kukosa hata siku moja
Kikosi kazi cha Globu ya Jamii kingependa kutoa shukrani
za dhati kwa wadau wote duniani kote kwa kampani mnayotupa kila saa, siku,
wiki, miezi na hadi sasa ikiwa ni MIAKA TISA kamili. Si jambo dogo,
ukizingatia katika safari hii njiani tumekutana na kila aina ya changamoto,
kubwa kuliko yote ikiwa ni kufanya kila tuwezalo kubakia hapa tulipo kwa
kufuata weledi pamoja na sera ya HATUBAGUI, HATUCHAGUI; ATAYETUZIKA HATUMJUI,
pamoja na kauli mbiu kwa wadau watoa maoni ya kuwa waangalifu kutochafua hali
ya hewa wala kujeruhi hisia ya mtu wakati wa kutoa maoni.
Katika kuadhimisha hii MIAKA TISA ya Libeneke, Globu
ya Jamii haitofanya sherehe ya pamoja na wadau kama ilivyotarajiwa. Badala yake
Ankal kajikakamua na kununua kajikeki na kukata na kula na familia kwa niaba ya
wadau. Ila ahadi yetu ni kwamba, panapo majaaliwa, sherehe kubwa itaandaliwa
mwakani wakati wa kuadhimisha MIAKA KUMI. Ni mapema mno kusema itakuwaje, ila
panapo uhai itakuwa SHEREHE KUBWA na inayostahili.
Globu ya Jamii pia inachukua nafasi hii kuwashukuru
wadhamini wake, ikiwa ni pamoja na VODACOM, AIRTEL, UHURU ONE, TTCL, NMB,
NBC, AZANIA BANK, CRDB, NHC, PRECISION AIR, AIR UGANDA, NSSF, PSPF, DSTV,
SKYLINK, SERENGETI FREIGHT FORWADERS ‘WAZEE WA KAZI’, SWIFT FREIGHT,
GIRAFFE OCEAN VIW HOTEL, DR MKOMBOZI, na wengineo wote. Tunashukuru kwa
kutuamini na kuendelea kuendeleza nasi Libeneke.
Washauri wakuu wetu pia hatuwasahau katika hili. Nao
ni Profesa Mark Mwandosya, Mhe. January Makamba, Freddy Macha, Balozi Peter
Kallaghe, Othman Michuzi, Ahmad Michuzi, Christopher Makwaia MK, Steve Wassira
jnr., Nathan Chiume, DJ Luke Joe wa Vijimambo, Waziri Ally, John Kitime, Alex
Perullo, Muhidin Maalim Gurumo, kaka Jeff Msangi, Boniface Makene, Kirk Gills,
Oscar Shelukindo, Ephraim Mafuru, Imani Kajula, Profesa Mbele, Da' Chemi
Chemponda, Ankal Beda Msimbe, kaka Assah Mwambene, Da' Tagie Daisy Mwakawago,
Shamim Zeze wa 8020 Fashions, Mama wa Mitindo Asia Idarous na mumewe Mzee
Khamsin, Ainde, kaka Asimwe Kabuga, Abdallah Ezza na Fide Tungaraza wa
Heslsinki na wengineo wengi tu. Ushauri wenu tunauthamini na kuuheshimu!
Wengine ni viongozi wote wakuu wa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Spika, Naibu Spika na maofisa wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wabunge wote wa Jamhuri ya
Muungano pamoja na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Viongozi maofisa wote
wa vyama vya siasa, Viongozi wote na watumishi wa taasisi za umma na
binafsi, Mablogger wote na mwisho ni wadau wote wanaotupa moyo kila kukicha.
Asanteni sana, sana, sana, sana. Hatuna cha kuwapa zaidi ya hizo
SHUKURANI kutoka katika kilindi cha moyo wetu. MOLA AWE NANYI, NA AWAZIDISHIE
PALE PALIPOPUNGUA.
Hatuna la zaidi la kusema zaidi ya kuahidi kwamba
tutaendeleza Libeneke kwa moyo wetu wote huku tukipiga magoti kuwaomba wapendwa
wadau wetu duniani kote muendelee kutupa kampani, kwani bila ninyi sisi si
lolote si chochote. Pia tunaomba radhi pale tunapoteleza kama binaadamu yeyote
ambaye daima duni si mkamilifu, ambapo likitokea litalotokea si kwa makusudi
ama nia mbaya bali ni kwa udhaifu huo huo wa kibinaadamu.
Naomba kuwasilisha,
Wenu Mnyenyekevu,
Muhidin Issa Michuzi “Ankal”
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako