Wakili wa serikali Mkuu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Frederick Manyanda (kulia) akieleza kwa waandishi (hawapo pichani) mkakati wa kuhakikisha kuwa huduma ya usimamizi na utoaji wa haki inawafikia wananchi wote kwa karibu kwa kufungua ofisi zaidi Mikoani, Katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Jijini Dar es Salaam,katikati ni Afisa Habari toka ofisi hiyo Bi. Asiatu Msuya na kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Bi. Georgina Misama.
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
YAFUNGUA OFISI 23 KATIKA MIKOA MBALIMBALI KUFANIKISHA MPANGO WA
UTENGANISHWAJI WA SHUGHULI ZA UPELELEZI NA UENDESHAJI WA MASHTAKA NCHINI
Utangulizi
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
imefanikiwa kufungua Ofisi 23 katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga,
Kilimanjaro (Moshi), Arusha, Mwanza, Kagera (Bukoba) Mara (Musoma), Shinyanga,
Tabora, Singida, Iringa, Mbeya, Mtwara, Lindi, Dodoma, Rukwa
(Sumbawanga),Ruvuma (Songea), Njombe,
Manyara,Morogoro,Kigoma,Geita na Pwani. Aidha jumla ya Ofisi mbili
(2) za zimefunguliwa katika Wilaya za Temeke na Monduli. Kwa mwaka wa
fedha 2012/2013 pekee jumla ya Ofisi tano (5) zimefunguliwa katika mikoa ya
Pwani, Kigoma, Morogoro, Manyara, Njombe na Geita ikiwemo pia Ofisi mbili za
Wilaya.
Lengo
Lengo kuanzishwa na kuimarishwa
kwa Ofisi hizi za Mikoa na Wilaya ni kuhakikisha kuwa huduma ya usimamizi na
utoaji wa haki inawafikia wananchi wote kwa karibu zaidi. Baadhi ya huduma
zinazotolewa ni pamoja na kuendesha Mashtaka mahakamani, kushughulikia
malalamiko na kero za wananchi kuhusiana na kesi za jinai na madai
zinazowakabili, kutembelea mahabusu na kuratibu upelelezi wa kazi za upelelezi
wa makosa ya jinai zinazofanywa na vyombo pelelezi/chunguzi ikiwemo Polisi,
Magereza, Uhamiaji,TAKUKURU.
Utekelezaji wa Mpango wa kutenganisha
Upelelezi na Mashtaka nchini
Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali imeendelea kutekeleza mpango huu wa Utenganishwaji wa
Upelelezi na Mashtaka kwa mujibu wa Sheria ambapo mfumo wa Sheria ambao
uliwezesha kutungwa kwa Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, 2005 na Sheria ya
Usimamizi wa Uendeshaji Mashtaka nchini, 2008 umeboreshwa; pamoja na kuanzishwa
kwa Jukwaa la Ki-taifa la Haki-Jinai (National Criminal Justice Forum) Desemba
2009 linaloviunganisha pamoja vyombo vyote vinavyosimamia utolewaji wa
Haki-Jinai nchini;
Serikali pia
imeboresha Muundo wa Divisheni ya Mashtaka kwa kuweka Sehemu
(Section) mahsusi inayosimamia utekelezaji wa mchakato wa utenganishaji wa kazi
za upelelezi na Mashtaka na uratibu wa kazi za ki-pelelezi; pamoja na
kuanzishwa kwa huduma ya Mashtaka ya moja kwa moja ambako Mawakili wa Serikali
wanaendesha kesi; Hii imepelekea idadi ya kesi zinazofunguliwa
Mahakamani ambako Mawakili wa Serikali wanaendesha Mashtaka kupungua
ikilinganishwa na kipindi cha nyuma; Kuongezeka kwa ubora wa huduma zitolewazo
na kupungua kwa kesi za kubambikizwa.
Utekelezaji wa Programu ya
Utenganishwaji wa Mashtaka na Upelelezi (Civilianization) imetoa msukumo mkubwa
kwa Ofisi kuingia uanachama na makubaliano ya mashirikiano na vyama
vinavyohusiana na kazi za Uendeshaji Mashtaka duniani, kama vile-IAP, HOPAC,
APA, EAAP, na ARINSA; Serikali
itaendelea kupanua wigo wa uendeshaji wa Mashtaka kwa kuanzisha na kuimarisha
Ofisi katika Wilaya zote nchini pamoja na Mikoa miwili iliyobaki ya Katavi na
Simiyu.
Tunapenda kuwakumbusha Wadau wetu wote
na Wananchi kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za uhalifu au
jinai yoyote katika jamii kwa vyombo husika kupitia utaratibu unaofaa; na kutoa
ushahidi Mahakamani pale unapohitajika kwa kuwa hizi ni nguzo muhimu
katika uendeshaji wa kesi mbalimbali. Aidha tunatoa wito kwa umma, wadau wetu
na wananchi wote kwa ujumla pamoja na vyombo vya habari nchini kufuatilia
mtiririko, hoja zinazowalishwa Mahakamani na uamuzi uliotolewa na Mahakama
katika kesi mbalimbali zinazoendelea kuwa na taarifa sahihi ya kuhusu kesi
hizo.
Imetolewa Na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali
Ijumaa, Septemba 27, 2013
Kwa mawasiliano zaidi
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
SLP 9050
KIVUKONI FRONT
DAR ES SALAAM
SIMU: +255 22 21181778
NUKUSHI: +255 22 2113236
BARUA PEPE: info@agctz.go.tz
TOVUTI: www.agctz.go.tz
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako