Mahakama moja nchini Misri, imeamuru kufungwa kwa vituo vinne vya
televisheni, ambavyo vimetuhumiwa kupendelea chama cha Muslim Brotherhood.
Vituo hivyo ni
pamoja na kituo cha chama hicho, Ahrar 25 na tawi la kituo cha Al-Jazeera
kinachopeperushia matangazo yake nchini Misri.
Wakati huohuo,
jeshi la Misri, limefanya mashambulizi ya angani dhidi ya maeneo yanayoshukiwa
kuwa ngome za wapiganaji wa kiisilamu katika rasi ya Sinai na kumuua mtu mmoja.
Jeshi
linajaribu kuonyesha kuwa lina udhibiti wa eneo hilo linalopakana na Gaza.
Kufungwa kwa
vituo hivyo, kunakuja baada ya serikali kufanya msako dhidi ya vyombo vya
habari vinavyoonekana kuunga mkono rais aliyeondolewa mamlakani Mohammed Morsi,
aliyepinduliwa na jeshi tarehe 3 mwezi Julai.
Vituo kadhaa
pia vililazimia kufunga kufuatia hatua za kijeshi.
Sasa mahakama
mjini Cairo, imeamuru stesheni ya Al-Jazeera, Mubashir Misr kufungwa na Ahrar
25 pamoja na vituo vingine Al-Quds na Al-Yarmuk.
Siku ya
Jumatatu , Misri iliwafurusha waandishi watatu wa habari wa kigeni waliokuwa
wanafanya kazi na Al-Jazeera ikisema kuwa hawakuwa na stakabadhi zinazohitajika
kufanya kazi nchini humo.
Bwana Morsi
amezuiliwa akisubiri kufunguliwa mashtaka.
Viongozi wa
mashtaka walitangaza wiki jana kuwa atashtakiwa kwa kosa la kuchochea mauaji ya
waandamanaji mwaka jana.
Vuguvugu la
Muslim Brotherhood limeitisha maandamano chini ya kauli mbiu 'Mapinduzi ni
ugaidi'.
Shirika la habari la
serikali Mena, linasema kuwa maafisa wa usalama wameziba baadhi ya barabara
huku magari ya kijeshi yakisemekana kuziba sehemu za kuingilia medani ya Rabaa
al-Adawiya na Tahrir.
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako