CHAMA cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kimeendelea kuwavuta wasanii kujiunga na chama hicho,
ambapo sasa wasanii wanne wa muziki wa kizazi kipya, maarufu Bongofleva na
filamu, wanatarajiwa kutangazwa kuhamia chama hicho wiki hii.
Wasanii hao wanadaiwa tayari
kukubali kuingia kwenye chama hicho na wanatarajiwa kutangazwa rasmi hadharani
katika mkutano wa hadhara utakaofanyika jijini Dar es Salaam.
Kukubali kwao kuingia katika
siasa, kunatajwa kutokana na ushawishi mkubwa uliofanywa na wabunge vijana wa
chama hicho, pamoja na Diwani wa CCM kutoka kata moja ya Wilaya ya Kinondoni,
ili chama hicho kivune kura za vijana katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Wabunge hao wa Chadema na
majimbo yao katika mabano ni Halima Mdee (Kawe); Kabwe Zitto (Kigoma
Kaskazini); John Mnyika (Ubungo) na Joseph Mbilinyi, jina la kisanii Sugu
(Mbeya Mjini).
Habari kutoka kwa watu wa
karibu na wasanii hao pamoja na ndani ya Chadema, zinawataja wasanii hao kuwa
ni wanamuziki Judith Wambura maarufu Lady Jaydee na wa miondoko ya Hip hop,
Selemani Msindi ama Afande Sele.
Taarifa zinawataja wengine kuwa
ni mwanamuziki Fredy Maliki maarufu Mkoloni na mwigizaji wa filamu, Jacob
Steven kwa jina la kisanii JB.
Inadaiwa wasanii hao lengo la
kuingia katika siasa kupitia chama hicho, ni kuwania ubunge ambapo Jaydee
anatajwa kutaka kugombea wilayani Musoma; Afande Sele Morogoro Mjini; Mkoloni
Jimbo la Tanga na JB Jimbo la Mkoa wa Dar es Salaam.
Hata hivyo walipotafutwa kuzungumzia taarifa hizi wengine walikana ingawa wapo waliokiri
kushawishiwa kuingia kwenye chama hicho na viongozi wa Chadema na wananchi, ili
wagombee ubunge.
Afande Sele alikana
kujiunga na chama hicho na kusema hana taarifa hizo isipokuwa ni kweli
ameshawahi kufuatwa na viongozi wa Chadema wa Mkoa wa Morogoro, wakimtaka
ajiunge na chama hicho na agombee ubunge Morogoro Mjini.
“Nimeshafuatwa na viongozi wa
Chadema wa mkoa na kata nijiunge na chama hicho na nigombee ubunge …tena hata
vijana wengi na baadhi ya wazee wamenitaka nigombee ubunge kwa kupitia Chadema
lakini nimekataa.
“Pia Sugu ni mshikaji wangu na
anapokuja Morogoro, vijiwe vyake ndio vyangu naye vijana wameshamfuata
wakimwambia anishawishi nigombee ubunge kupitia Chadema, amekuwa akiniambia
vijana wananitaka lakini mimi sitaki, sijawahi kujiunga na chama chochote na
naona mbunge wa sasa (Abdulaziz Aboud) anafanya kazi nzuri.
“Mimi sio mwanasiasa, lakini ni
mwanaharakati kupitia muziki na mtandaoni na nimekuwa nikitoa maoni mengi na
kukosoa lakini narudia si mwanasiasa na sijawahi kujiunga na chama chochote,”
alisema Afande Sele.
Vilevile amekanusha
kushawishiwa na viongozi wa kitaifa wa Chadema au wabunge, ingawa amekiri kuna
wabunge wa chama hicho kuwa ni marafiki zake wakiwemo Mbilinyi na Zitto.
Kwa upande wa Jaydee alisema
hafuati itikadi ya chama chochote cha siasa na hapendi siasa kutokana na imani
kuwa siasa ni uongo na yeye hapendi uongo. Alisema hana nia ya kujiunga na
chama chochote cha siasa wala kugombea ubunge kupitia chama chochote.
Hata hivyo alipoulizwa iwapo
atagombea baada ya Katiba kuruhusu mgombea binafsi, alisema kwa wakati huo
atajua.
Hata hivyo, Licha ya kuwaona
wanasiasa ni waongo, anakiri wapo wanasiasa anawaamini kutokana na kazi zao na
kumtaja miongoni mwao ni Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na Mbunge wa Afrika
Mashariki, Shy-rose Bhanji.
Mwanamuziki huyo alisema licha
ya kuwa na marafiki wa Chadema na CCM kama Sugu na Profesa Jay wa Chadema na
Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige na Bhanji wa CCM, hawajawahi
kumshawishi kujiunga na vyama vyao.
Mkoloni Akizungumzia taarifa
hizo za kujiunga na Chadema, JB alikana na kusema; “mimi na siasa ni vitu viwili
tofauti”
Kwa upande wa Mkoloni, alisema
hajawahi kufuatwa wala kushawishiwa kujiunga na chama chochote, isipokuwa ni
mwanachama wa muda mrefu wa Chadema na amekuwa akishiriki kampeni, mikutano ya
hadhara na matukio yote ya uhamasishaji ndani ya chama hicho.
Alisema kuhusu kuombwa kuwania
jimbo mkoani Tanga kwa tiketi ya chama hicho, alisema hajawahi kuombwa na chama
hicho kufanya hivyo.
“Sijawahi kuombwa nigombee
jimbo, na kuhusu nia ya kugombea, ni mapema mno kuzungumzia suala hilo sasa na
hata kanuni za chama changu haziruhusu labda uniulize swali hilo mwakani naweza
kuwa na jibu,” alisema Mkoloni.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa, alikataa kuzungumzia taarifa hizo akidai yuko
barabarani na masuala yote yanayohusu chama hicho aulizwe Msemaji wa chama
hicho.
Hata hivyo msemaji wa chama
hicho, Tumaini Makene alisema hana taarifa kuhusu kufanyika kwa mkutano wa
chama hicho Dar es Salaam na kutaka apewe muda afuatilie taarifa hizo kwa
makini zaidi.
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako