Saturday 9 November 2013

TIDO MHANDO AMUUMBUA JUMA NKAMIA



MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Tido Mhando, amemuumbua Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM), akisema ni mbumbumbu wa taaluma ya uandishi wa habari. Tido alirusha kijembe hicho jana, wakati akizungumza katika hafla ya kutolewa kwa tuzo ya uandishi wa kishujaa na utumishi uliotukuka ya Daudi Mwangosi, iliyoandaliwa na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC), jijini hapa.
Tido, ambaye aliwahi kufanya kazi katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), akiwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili na baadaye Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), alimshangaa Nkamia kwa kusema maneno ya uongo bungeni.

 

 Katika mkutano wa Bunge uliopita, Nkamia aliwakashifu waandishi wa habari akisema hawajui habari ni nini, huku akijigamba kuwa yeye ni mwandishi mkongwe aliyefanya kazi katika vyombo vikubwa vya habari duniani.
Katika mchango wake bungeni, Nkamia alitaja baadhi ya vyombo alivyofanyia kazi na kueleza kuwa akiwa BBC, alifanya kazi katika kitengo cha propaganda.

“Kuna mbunge mmoja ambaye anajiita kuwa alikuwa mwandishi wa habari, amekuwa kila mara anaposimama kwenye vikao vya Bunge anatoa maneno ya kashfa kwa waandishi na kusema kuwa yeye anawajua sana waandishi.
“Ni vema akaeleza ukweli ni kwanini alitoka BBC, pia awaeleze kama aliajiriwa BBC kama mwandishi au alichukuliwa kwenda kusoma habari na mimi ndiyo nilikuwa bosi wake.
“Hicho kitengo anachodai kuwa ni cha propaganda alichowahi kufanya kazi BBC hakipo na ni uongo ambao amekuwa akiwadanganya watu na kuendelea kudhalilisha taaluma ya habari,” alisema.
Tido alisema kuongezeka kwa makanjanja katika fani ya habari kunatokana na baadhi ya watu wanaojiita waandishi kuvamia taaluma ya habari, huku wakitambua kuwa hawajasomea taaluma hiyo.
Katika hotuba yake hiyo, Tido aliwataka wanahabari kutambua kuwa umefika wakati sasa wa kukataa kutumiwa na wanasiasa na viongozi mbalimbali wa serikali na wafanyabiashara kwa kukubali kupokea fedha na bahasha, jambo ambalo ni hatari.

“Wananchi wanatutegemea kuibua mambo mengi ya ufisadi, rushwa, wizi na hata ujangili, ikiwemo ya uhalifu na uhamiaji haramu kushika kasi ndani ya nchi yetu.

“Waandishi tuwe majasiri kufichua hayo kwa kuandika ukweli na bila kupotosha umma, ili jamaii inayotutegemea iweze kutuamini na kutupa ushirikiano wa dhati katika kutekeleza majukumu yetu kwa uhakika zaidi,” alisema.
Mwangosi ambaye alikuwa mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, aliuawa Septemba 2, mwaka jana, mikononi mwa polisi katika Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi, Mkoa wa Iringa

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako