ROSTAM AZIZ |
BILA kutarajiwa na watanzania wengi mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz (49), ametajwa kuwa ndiye tajiri namba moja Tanzania kwa sasa.
Kwa mujibu wa
utafiti uliofanywa na Jarida la Marekani la Forbes na kutoa taarifa yake hiyo,
Rostam amekamata nafasi hiyo na ya 27 katika Afrika akiwa na utajiri wa Dola za
Marekani bilioni moja Sh1.6 trilioni.
Mbunge huyo wa
zamani wa Igunga, ameingia kwa mara ya kwanza katika orodha ya matajiri 50 wa
Afrika ya jarida hilo, pamoja na wafanyabiashara wengine wa Tanzania, Reginald
Mengi na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohamed Dewji 'Mo'. Katika orodha hiyo
pia yumo Said Bakhresa ambaye aliwahi kutajwa siku za nyuma.
Rostam, ambaye
aliachana na siasa mwaka 2011, amempiku Bakhresa, ambaye mwaka jana Jarida la
Ventures Africa la Nigeria lilimtaja kuwa ndiye aliyekuwa tajiri namba moja wa
Tanzania. Bakhressa katika kipindi hicho alikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola
620 milioni (Sh971 bilioni).
Katika orodha hiyo
ya Ventures Africa, Bakhresa alifuatiwa na Rostam, Mengi na mfanyabiashara
mwingine maarufu, Ali Mufuruki.
Mengi anashika
nafasi ya pili kwa Tanzania na ya 34 Afrika akiwa na utajiri wa Dola 550
milioni (Sh861 bilioni).
Forbes linaonyesha
kuwa Bakhresa amefungana na Mo katika nafasi ya tatu ya orodha ya matajiri wa
Tanzania na ya 38 kwa Afrika, wote wakiwa na utajiri wa Dola 500 milioni (Sh783
bilioni).
Rostam, Mengi na
Bakhresa hawakupatikana kuzungumzia suala hilo huku Mo akisema kwamba
asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa kuwa jana alikuwa katika mapumziko ya
Sikukuu ya Ashura.
Tajiri wa Nigeria,
Aliko Dangote, ambaye anajenga Kiwanda cha Saruji huko Mtwara ndiye anayeshika
nafasi ya kwanza katika orodha ya Afrika, akiwa na utajiri wa Dola20 bilioni
(Sh31.7 trilioni), akifuatiwa na familia ya Johanny Rupert ya Afrika Kusini
yenye utajiri wa Dola7 bilioni (Sh10.7 trilioni) na Nick Oppenheimer, pia wa
Afrika Kusini mwenye utajiri wa Dola 6.6 bilioni (Sh10.3 trilioni).
1)Rostam Aziz
Jarida la Forbes
limeripoti kuwa utajiri wa Rostam unachangiwa zaidi na biashara ya mawasiliano
ya simu za mkononi, ujenzi na uchimbaji wa madini.Pia anamiliki Kampuni ya
Caspian, ambayo inafanya kazi za kuchimba madini katika migodi inayomilikiwa na
Kampuni za BHP Billiton na Barrick Gold.
Pia ana hisa
katika Kampuni ya Hutchison Wampoa inayofanya kazi za kupakua mizigo bandarini
na anamiliki majumba nchini na katika nchi za Mashariki ya Kati.
2) Mengi
Ni Mwenyekiti
Mtendaji wa Kampuni za IPP.
Utajiri wake
unatokana na kumiliki vyombo vya habari, kiwanda cha vinywaji baridi na madini.
Mengi anamiliki
magazeti kumi na moja, vituo vitatu vya televisheni na takriban vituo 10 vya
redio.
Pia ana mgodi wa
madini ya dhahabu na viwanda vya CocaCola.
Kwa mujibu jarida
hilo, Mengi alizaliwa katika familia maskini na baadaye kusomea uhasibu huko
Uingereza na kufanya kazi huko.
Alijiunga na Chama
cha Wahasibu cha Uingereza kabla ya kurejea Tanzania mwaka 1971 na kuajiriwa na
Kampuni ya Ukaguzi ya Coopers & Lybrand Tanzania (sasa Price Water House
Coopers) hadi mwaka 1989, alipoacha kazi na kujikita zaidi katika biashara.
3) Bakhresa
Said Salim
Bakhresa ni mwasisi na Mwenyekiti wa Kampuni ya Bakhresa Group na ana utajiri
wa Dola500 milioni (Sh783 bilioni).Bakhresa aliacha shule akiwa na umri wa
miaka 14 na kuanza biashara ya kuuza viazi mbatata. Baada ya hapo alifungua
mgahawa na baadaye kuingia katika biashara ya kusaga nafaka.
4) Mo
Mafanikio yake
yamechangiwa zaidi baada ya kuendeleza mali ya wazazi wake. Anafanya biashara
ya nyumba, kuuza mazao na viwanda vya mafuta.
Mo alirejea
Tanzania baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Georgetown,
Marekani na kuendeleza biashara ya maduka ambayo yalianzishwa na baba yake.
Alinufaika baada
ya kununua viwanda vilivyobinafsishwa na Serikali.
Alivifanya viwanda
hivyo kutengeneza faida na kuinyanyua Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL)
kuwa miongoni mwa kampuni zenye mafanikio makubwa Tanzania.
Mo pia
anajihusisha na biashara ya usambazaji bidhaa, viwanda vya nguo na kilimo.
Jarida hilo
lilipiga hesabu za utajiri wa wafanyabiashara hao kwa kuangalia thamani ya
bidhaa zinazouzwa na kampuni zao, mikataba yao na hasa wale walio kwenye sekta
ya mafuta na ukubwa wa kampuni zao.
No comments:
Post a Comment
Ahsante kwa Maoni yako