Wednesday 6 November 2013

MAGHOROFA 64 HATARI KWA AFYA ZA WAKAZI WA DAR



Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Design Plus Architects, Mustafa Maulid akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu ukaguzi wa majengo 67 yaliyojengwa kinyume na utaratibu na chini ya kiwango eneo la Kariakoo. Kushoto ni Mhasibu wa Kampuni hiyo, Zaina Nassor. 

Maghorofa 64 yaliyopo eneo la Kariakoo, Manispaa ya Ilala yamejengwa kinyume na sheria na kwamba baadhi yanaweza kuporomoka kutokana na ujenzi wake kuwa chini ya kiwango.
Kampuni iliyopewa zabuni ya kufanya ukaguzi wa majengo Manispaa ya Ilala, inayoitwa Design Plus Architects (DPA) imebaini kati ya majengo ya ghorofa 90 yaliyokaguliwa, 67 yamejengwa kinyume na sheria.
Uamuzi wa kuipa kampuni binafsi kazi ya kukagua majengo, ulikuja baada ya jengo la ghorofa 16 kuanguka na kuua watu 36 Machi 26, mwaka huu.
Meneja Uendeshaji wa DPA, Mustafa Maulid alisema jana kwamba ukaguzi wa majengo hayo ulianza Julai mwaka huu baada ya kupata zabuni hiyo.
"Hali ni mbaya katika majengo tuliyoyakagua, kuna majengo ya ghorofa yenye nyufa nyingi, pia yapo majengo yanayogusana ambayo ni hatari kwa watumiaji," alisema.
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa alipoulizwa hatua za kuchukua, alisema vikao vya madiwani vitaamua hatua za kuchukua baada ya kuipitia ripoti ya ukaguzi huo.
"Ukipita Kariakoo hata kama siyo mtaalamu wa ujenzi utagundua kwamba majengo mengi yamejengwa bila kufuata sheria za ujenzi, baada ya kuanguka kwa jengo katikati ya jiji, tukaamua kuipa kampuni binafsi kazi ya ukaguzi ili kuona ni majengo gani yapo kinyume na sheria," alisema Silaa.
Akifafanua zaidi, Maulid alisema makosa waliyoyabaini ni watu kuendesha ujenzi bila kuwa na vibali.
Alisema makosa mengine ni ujenzi bila kufuata michoro iliyoidhinishwa na Manispaa ya Ilala.
"Hii ina maana kwamba watu wanajenga majengo tofauti na michoro inayotoka kwa wataalamu wa manispaa. Kwa mfano majengo yote Kariakoo yanatakiwa kuwa na maegesho ya magari lakini wao wanaweka flemu za maduka," alisema Maulid.
Pia, alisema watu wanahamia kwenye maghorofa kabla hayajaisha kitendo ambacho ni kinyume na sheria.
Kuhusu changamoto walizokutana nazo, Maulid alisema baadhi ya wamiliki wa nyumba walikuwa wakiwazuia kuingia kufanya ukaguzi, huku wengine wakikimbilia kushtaki kwa wanasiasa.
Alisema wengine wamekuwa wakiwatishia kwa lengo la kuwazuia kufanya kazi hiyo na kwamba, wataendelea na kazi hiyo hadi wamalize.
Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako