Monday 11 November 2013

KENYA WAIPONGEZA TANZANIA JUU YA KUJITOA JUMUIYA AFRIKA MASHARIKI

BI AMINA MOHAMED WAZIRI WA MAMBO YA NJE NCHINI KENYA

KENYA imekuwa nchi ya kwanza kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki kuipongeza Tanzania kwa hatua yake ya kutangaza bayana kwamba haiko tayari kutoka katika jumuiya hiyo kama ilivyodhaniwa.
Wasiwasi kuwa Tanzania ingejitoa kutoka jumuiya ya Afrika Mashariki ulitokana na hali iliyojitokeza kwa baadhi ya nchi za jumuiya hiyo kuendesha mikutano yao bila kuishirikisha Tanzania na Burundi.
Baadhi ya wanasiasa na wananchi nchini Tanzania walitaka nchi yao iachane na jumuiya hiyo wakizishutumu Kenya, Rwanda na Uganda kuitenga Tanzania hata katika mikutano ya masuala yaliyohitaji maamuzi ya jumuiya.
Kufuatia mfarakano huo, ulionekana kutishia uhai wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, wiki hii alilihutubia bunge la Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, katikati ya nchi na kutangaza bayana kuwa Tanzania haitatoka katika jumuiya ya Afrika Mashariki, kwani imefanya kazi kubwa kuifufua na kuiunda upya baada ya kusambaratika mwaka 1977.
Kwa upande wake, Kenya moja ya nchi waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na ambayo ilishutumiwa kushiriki kuibagua Tanzania, imemtuma waziri wake wa mambo ya nje, Amina Mohammed kwenda Tanzania na kuwa na mazungumzo na waziri mwenzie wa mambo ya nje Bernard Membe kuhusu mfarakano huo na nia ya kuimarisha zaidi uhusiano wa nchi mbili hizo.
Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jumapili, waziri Amina Mohammed, amesema Kenya inaunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, kuhusu uamuzi wake wa kutojitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku akisisitiza kuwa bila Tanzania hakuna Afrika Mashariki na bila Afrika Mashariki hakuna Tanzania.
"Kama unavyojua Kenya na Tanzania tumekuwa tukiijenga jumuiya ya Afrika Mashariki kwa muda mrefu sana, tuko na mafanikio mengi sana, kuna mambo mengi tumeyafanya, kuna njia ndefu imebakia kuna mambo mengi yasiyoweza kupimwa kati ya nchi hizi. Na tuna tumaini kwamba tutaendelea kuijenga Afrika Mashriki kwa nguvu zote na tutawasiliana na watu wetu kwa sababu tunataka watu wetu waishi vema na wawe majirani wazuri na waendelee . Kwa Tunataka uchumi wetu uende vizuri. Kwa hiyo tutaendelea kushirikiana, sisi ni wale wa kwanza tuliokuwa pale kwa hiyo tunataka tufanye kile tunachoweza kuendeleza Afrika Mashariki..... Lakini tumefurahia sana sana hotuba ya Rais aliyotoa pale bungeni na tunawashukuru pia Watanzania kumuunga mkono."
Uhusiano wa Kenya na Tanzania ni wa kindugu
Pia waziri Amina amesisitiza kuwa hakuna namna ambavyo Tanzania na Kenya zitatenganishwa, kwa namna ambavyo zimejenga maingiliano makubwa ya kijamii na kiuchumi, huku akiomba Tanzania kusaidia kusukuma ombi la Kenya la kutaka kesi ianyomkabili Rais wake, Uhuru Kenyatta iahirishwe kwa mwaka mmoja zaidi ili kumpa fursa ya kutekeleza majukumu yake ya kitaifa.
Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Benard Membe amesema serikali yake imefurahi kuona Kenya imekuwa nchi ya kwanza kuipongeza Tanzania kwa kuinusuru jumuiya ya Afrika Mashariki kama ilivyokuwa mwanzoni na kujenga jumuiya ya watu na si ya viongozi, na kuahidi kushirikiana na Kenya katika masuala mbalimbali likiwemo la kutaka kesi inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta katika mahakama ya ICC iahirishwe kwa mwaka mmoja zaidi.
Waziri Membe amesema waziri mwenzake Amina kutoka Kenya amesema hotuba ya Rais Kikwete imewazindua kwani hawakujua kuwa baadhi ya yale waliyokuwa wakiyafanya yalikuwa ni kukiuka taratibu za Jumuia ya Afrika Mashariki na kuahidi kuwa Kenya itashirikiana kikamilifu na nchi waanzilishi halisi wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
DK JAKAYA KIKWETE RAIS WA TANZANIA
 Katika kuonyesha nia thabiti ya kutotoka katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Kikwete katika hotuba yake aliyoitoa bungeni, alisema "Tanzania ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na mwaminifu na tunatimiza wajibu wetu kwa jumuia na kuhusika kikamilifu katika ujenzi wake."alisema.
Rais Kikwete alitumia muda mrefu katika hotuba hiyo kuchambua masuala mbalimbali ya msingi ya uhai wa jumuia hiyo huku akisema ameshangazwa na nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kuzitenga Tanzania na Burundi.

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako