Monday 9 February 2015

HONGERA IVORY COAST KWAKUWA MABINGWA WAPYA WA AFCON


Timu ya taifa ya soka ya Ivory Coast imefanikiwa kuunyakua ubingwa wa mataifa ya Afrika kwa mara ya pili, baada ya kuibwaga Ghana 'Black Stars' katika mechi ya fainali iliyochezwa nchini Equatorial Guinea. Kwenye pambano hilo kali na la kusisimua  lilimalizika katika dakika 90 za mchezo, huku timu zote mbili zikitoka sare ya bila ya kufungana.
 Muda wa dakika 30 za nyongeza nao haukuweza kumtoa mshindi wa pambano hilo. Baada ya kumalizika dakika 120 za mchezo, ulichukuliwa uamuzi wa kupigiana penalti  tano – tano, na hapo ikajirudia historia ya fainali ya mwaka 1992.
 Ivory Coast ilianza kupoteza penalti zake mbili, huku Ghana wakiwa na matumaini ya kuibuka na ushindi, lakini Ivory Coast ilianza kujirekebisha katika upigaji wa penalti, na Ghana nao wakaharibu mikwaju yao miwili, lakini baada ya kuendelea michomo ya funga nikufunge, hatimaye kipa wa Ivory Coast alizuia mkwaju wa kipa wa Ghana, na kutandika mkwaju wa tisa na kuibeba Ivory Coast kwa ushindi wa mabao 9-8.
Mchuano huo ulirejesha historia ya fainali ya mwaka 1992, ambapo Ivory Coast iliutwaa ubingwa huo kwa kuifunga Ghana kwa mikwaju ya penalti 12 kwa 11. Ghana imeshalinyakua kombe la mataifa ya Afrika mara tano. Siku ya Jumamosi, ilichezwa mechi ya kumtafuta mshindi wa tatu wa michuano hiyo kati ya wenyeji Equatorial Guinea ilipokamuana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo Kongo ilishinda kwa penalti 4-2.

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako