Thursday 5 February 2015

YANGA YABANIWA NA TFF



SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limekataa ombi la Yanga SC kutaka mchezo wao na Mtibwa Sugar uahirishwe ili wapate fursa nzuri ya maandalizi ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya BDF XI ya Botswana.

Na kwa sababu, hiyo Yanga SC wanaondoka asubuhi ya leo kurejea kambini kwao, Bagamoyo kuendelea na maandalizi ya mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Yanga SC watacheza mechi ya tatu ndani ya wiki moja Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya mabingwa wenzao wa zamani wa Ligi Kuu, baada ya Jumapili iliyopita kulazimishwa sare ya 0-0 na Ndanda FC na jana kushinda 1-0 dhidi ya Coastal Union.

Yanga SC ilipanda kileleni mwa Ligi Kuu jana kufuatia ushindi huo wa ugenini, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa kutimiza pointi 22 baada ya kucheza mechi 12, moja zaidi ya mabingwa watetezi, Azam FC wanaoshika nafasi ya pili kwa point 21.

Shujaa wa pointi tatu za Yanga SC jana alikuwa ni Nahodha Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’, aliyefunga bao hilo pekee mapema tu kipindi cha kwanza, baada ya kupanda kwenda kusaidia mashambulizi.

Ilikuwa ni dakika ya 12 ya mchezo, wakati Cannavaro alipomalizia kwa kichwa mpira wa kurushwa wa beki Mbuyu Twite na kuipandisha kileleni Yanga SC.

Baada ya mchezo na Mtibwa Sugar Jumapili, Yanga SC itakwenda kuweka kambi visiwani Zanzibar kujiandaa na mchezo wa kwanza, Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho Afrika.
@@@@@@@@@@@@@@@

No comments:

Post a Comment

Ahsante kwa Maoni yako