Mwezi Februari mwaka huu Super D atakuwa na ugeni mkubwa
wa bondia Mtanzania anayefanya kazi zake nchini Deer Park, Victoria,
Australia, Omari Kimweri ambaye anatua nchini kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa
wanamasumbwi wa Tanzania.
Akizungumza jijini Dar es salaam hapo jana, Super D
alisema kuwa ujio wa Kimweri ni fursa nyingine adimu kwa mabondia wa Tanzania
katika kuona ni vipi wanaweza kutimiza ndoto zao za kutoka kimaisha kupitia
mchezo huo.
Amesema kuwa Kimweri atatua akiwa na vifaa mbalimbali vya
masumbwi ambapo pia atatoa mafunzo na mbinu mpya zinazotumiwa na mabondia wa
nje pamoja na kushuhudia mapambano kadhaa yatakayofanyika kwa kipindi
atakachokuwapo hapa nchini.
“Kimweri anakuja akiwa na msafara wa watu kadhaa, akiwamo
mwanasoka wa kike, Melanie Gines ambaye ni raia wa Hispania. Akiwa hapa nchini,
Melanie atapata fursa ya kukutana na wanasoka wa kike wa hapa , kwani amechezea
timu nyingi za Ulaya, huko Hispania,”
Amesema kuwa ujio wa Kimweri umewezeshwa kwa kiasi
kikubwa na promota wake, Brian Amatruda ambaye ni miongoni mwa mapromota
maarufu nchini kwao Australia, akiwa amekubari kutoa baadhi ya vifaa vya kisasa
kutoka Hispania na Marekani kwa ajili ya ziara hiyo.
Super D anasema kuwa Kimweri ambaye ni bingwa wa WBO,
atatua nchini akiwa na mikanda yake yote aliyowahi kutwaa, ukiwamo wa ubingwa
wa Australia, lengo likiwa ni kuwahamasisha vijana wa kitanzania kujikita zaidi
katika ndondi.